Boulbina Aipeleka Algeria Robo Fainali Afcon 2025

Mshambuliaji wa akiba, Adil Boulbina, aliibuka shujaa wa Algeria baada ya kufunga bao la ushindi katika dakika za lala salama za muda wa nyongeza, na kuiongoza timu hiyo kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Morocco 2025, kufuatia ushindi mgumu wa bao 1-0 dhidi ya DR Congo.
Katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa, uliojaa nidhamu ya hali ya juu, nguvu na tahadhari kutoka kwa pande zote mbili, Boulbina alifunga bao hilo la pekee katika dakika ya 118, dakika tano tu baada ya kuingia uwanjani, na kuvunja moyo wa wapinzani waliokuwa wakijiandaa kwa mikwaju ya penalti.
Bao hilo lilipatikana baada ya Boulbina kupokea mpira upande wa kulia, akapiga chenga ya haraka kuingia ndani ya eneo la hatari, kisha akapiga shuti la kifundi lililomshinda kipa Lionel Mpasi-Nzau, ambaye kwa muda mrefu alikuwa mwiba kwa Algeria kutokana na uokoaji wake wa kuvutia.
Kwa kipindi chote cha dakika 90 pamoja na sehemu kubwa ya muda wa nyongeza, timu hizo zilikuwa zimefutiana nguvu, kila moja ikijaribu kwa tahadhari kuepuka makosa, huku nafasi za wazi za kufunga zikiwa adimu.
Algeria ilianza mchezo kwa kasi, ikitawala umiliki wa mpira na eneo la mchezo, lakini ilijikuta ikipambana kuipenya ngome imara ya DR Congo iliyokuwa imepangwa vyema. Licha ya shinikizo la awali, Algeria ilishindwa kuunda nafasi nyingi hatari, huku Mpasi-Nzau akibaki bila kujaribiwa kwa kiwango kikubwa katika dakika za mwanzo.

Kwa upande wao, DR Congo walionekana kuwa hatari zaidi walipopata nafasi za kushambulia kwa kushtukiza. Cedric Bakambu alipata nafasi nzuri katikati ya kipindi cha kwanza, lakini alizuiwa na kipa Luca Zidane aliyefanya uokoaji mzuri. Kutokana na kona hiyo, Axel Tuanzebe alipiga kichwa kilichopita lango kwa umbali mdogo.
Bakambu aliendelea kuwasumbua walinzi wa Algeria, akipiga tena kichwa kutoka krosi ya Aaron Wan-Bissaka, lakini mpira ulipita pembeni ya lango kwa bahati mbaya.
Algeria walijibu mashambulizi hayo kabla ya mapumziko, pale Ibrahim Maza alipoanzisha shambulizi la kushtukiza, lakini shuti lake la chini lilipita karibu sana na goli, likiwanyima mashabiki wao furaha ya bao la mapema.
Kipindi cha pili kilifuata muundo uleule, Algeria wakimiliki mpira zaidi na DR Congo wakitumia mashambulizi ya kushtukiza. Dakika 12 kabla ya mechi kumalizika, Mohamed Amoura alikosa nafasi ya wazi baada ya kushindwa kuupinda mpira kumpita Mpasi-Nzau.
Upande wa pili wa uwanja, beki Zineddine Belaid aliokoa jahazi la Algeria kwa kuzuia shuti la karibu la Fiston Mayele, tukio lililowafanya mashabiki kushika nyoyo zao.
Mchezo ulipoingia muda wa nyongeza, uchovu ulianza kuwa dhahiri kwa wachezaji, lakini kasi na ushindani viliongezeka. Mpasi-Nzau aliendelea kuonyesha ubora wake kwa kuokoa mashuti mawili makali kutoka kwa Fares Chaibi na Baghdad Bounedjah, hali iliyodokeza kuwa mechi ingeenda kuamuliwa kwa penalti.

Hata hivyo, Boulbina alikuwa na mpango tofauti. Bao lake la dakika za mwisho liliwasha shangwe kubwa kwa wachezaji na mashabiki wa Algeria, huku likimaliza safari ya DR Congo katika mashindano hayo kwa uchungu.
Kwa ushindi huo, Algeria sasa imefuzu robo fainali ambapo itavaana na Nigeria katika pambano kali litakalofanyika Marrakesh, ikiwa ni sehemu ya safari yao ya kutafuta taji la pili la AFCON ndani ya miaka sita.
Kauli za Makocha na Wachezaji Zaibua Mjadala
Mchezaji Bora wa Mechi (TotalEnergies Man of the Match): Adil Boulbina yeye hakua na mengi zaidi ya kushukuru Mungu akisema kuwa “Awali kabisa namshukuru Mungu. Nawapongeza Algeria na mashabiki wetu. Niliingia uwanjani dakika za mwisho na nikafunga bao, lakini huu ni ushindi wa timu nzima, sio wangu peke yangu. Ni furaha kubwa kwa kikosi,” alisema Boulbina.
Naye Kocha Mkuu DR Congo, Sébastien Desabre alilia bahati kuwa haikua upande wao kwani walijitahidi kufanya kila kitu kwa usahihi “Tulifanya vizuri hasa kipindi cha pili baada ya mabadiliko, lakini kulikuwa na kuporomoka kidogo katika muda wa nyongeza. Tulicheza vizuri na kutoa maonyesho mazuri ya kiufundi, lakini bahati haikuwa upande wetu. Nawapongeza Algeria. Sina lawama kwa wachezaji wangu, walitoa kila walichokuwa nacho.”
Kwa upande wa Kocha Mkuu Algeria, Vladimir Petković yeye aliamini alistahili kuibuka na ushindi kutokana na ubora mkubwa ambao ulionyeshwa na kikosi chake kuanzia dakika ya kwanza huku akiwasifu vijana wake kwa kujituma na kuweka nidhamu ya mchezo mbele mpaka wakapata bao hilo.
“Naamini tulistahili kushinda kutokana na kiwango tulichoonyesha. Tulitawala sehemu kubwa ya mchezo, tulicheza kama timu, tukadhibiti presha na hatimaye tukapata bao la ushindi. Tumefuzu, hilo lilikuwa muhimu, sasa tunajipanga kwa mchezo mgumu dhidi ya Nigeria.”Alisema Petkovic

