Ahoua Atua Algeria: Jinsi Atakavyoisaidia Cr Belouzdad

Kama ilivyoripotiwa awali, aliyekuwa kiungo mshambuliaji mahiri wa Simba SC, Jean Charles Ahoua (23), sasa ametambulishwa rasmi kama mchezaji mpya wa klabu ya CR Belouizdad ya Algeria, hatua inayohitimisha safari yake yenye mafanikio ndani ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania.

Nyota huyo raia wa Ivory Coast anaondoka Msimbazi akiwa ameacha alama kubwa na kumbukumbu zisizofutika, baada ya kuonyesha kiwango cha juu cha ubunifu, ufundi na ufanisi uliomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji bora kabisa waliowahi kuichezea Simba katika miaka ya karibuni.
Msimu wa 2024/2025, Ahoua alikuwa kinara wa mabao na pasi za mabao Simba SC, huku pia akimaliza msimu huo akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kufunga mabao 16. Mafanikio hayo yalienda sambamba na mchango wake mkubwa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup), ambako alikuwa mchezaji tegemeo wa wekundu hao wa Msimbazi.

Uhamisho wake kwenda CR Belouizdad unatajwa kuwa ni matokeo ya ufuatiliaji wa muda mrefu uliofanywa na kocha mkuu wa klabu hiyo, Sead Ramovic, ambaye alimwona Ahoua mara kadhaa alipokuwa akiifundisha Yanga SC kabla ya kujiunga na mabingwa hao wa Algeria. Ramovic alivutiwa na uwezo wa Ahoua kusoma mchezo, kuunganisha safu ya kati na ushambuliaji pamoja na uwezo wake wa kufunga akiwa nje ya boksi.
Kwa upande wa CR Belouizdad, ujio wa Ahoua unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika mfumo wao wa uchezaji. Klabu hiyo, ambayo ni miongoni mwa vigogo wa soka la Afrika Kaskazini, imekuwa ikihitaji kiungo mshambuliaji mwenye uwezo wa kubeba mchezo, kutengeneza nafasi na kutoa tofauti katika mechi ngumu, hasa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ahoua ana sifa zinazomfaa kikamilifu soka la Algeria, ambalo linahitaji mchezaji mwenye nguvu ya mwili, akili ya haraka na nidhamu ya kiufundi. Mbali na ubunifu, ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao ya mbali, kupiga mipira ya adhabu na kona kwa usahihi, pamoja na kutoa pasi za mwisho zinazoweka washambuliaji katika nafasi nzuri ya kufunga.
Aidha, uzoefu alioupata Tanzania na kwenye michuano ya CAF utamsaidia kuhimili presha ya mashabiki wa CR Belouizdad, klabu yenye matarajio makubwa kila msimu. Ahoua anaeleweka kama mchezaji anayependa majukumu makubwa, jambo linalompa nafasi ya kuwa mhimili wa kikosi hicho katika muda mfupi.
Kwa upande wa Simba SC, kuondoka kwa Ahoua ni pigo, lakini klabu hiyo tayari imeanza hatua za kujaza pengo lake kwa kukamilisha usajili wa Libasse Gueye kutoka Senegal pamoja na Nickson Kibabage, wachezaji wanaotarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya kati kuelekea mzunguko wa pili wa ligi.

Ikumbukwe kuwa kabla ya kujiunga na Simba, Ahoua alikuwa Mchezaji Bora wa Mwaka 2024 wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, jambo lililothibitisha ubora wake hata kabla ya kutua Tanzania. Mafanikio aliyoyapata akiwa Simba yameongeza thamani yake sokoni na kumfungulia mlango wa kwenda kucheza katika ligi yenye ushindani mkubwa zaidi.
Kocha wa mpya wa klabu ya Simba Sc Steve Barker ameripotiwa kuruhusu kuondoka kwa Ahou licha ya kuwa na takwimu nzuri ambapo kocha huyo ameona mchezaji huyo hana tena moyo na ari ya kuitumikia Simba Sc.
Kwa ujumla, uhamisho wa Jean Charles Ahoua kwenda CR Belouizdad ni hatua kubwa katika taaluma yake ya soka. Ikiwa ataendeleza kiwango alichokionyesha Simba, hakuna shaka kuwa atakuwa nyota muhimu kwa klabu hiyo ya Algeria na huenda akawa miongoni mwa viungo bora katika ukanda wa Afrika Kaskazini ndani ya muda mfupi.
Safari mpya inaanza, macho ya mashabiki sasa yakimwangalia Ahoua kuona kama ataendelea kuandika historia nje ya Tanzania.
