Alonso Ampisha Álvaro Arbeloa Madrid

Klabu ya Real Madrid imemtangaza rasmi Álvaro Arbeloa (42) kuwa kocha mkuu mpya wa kikosi cha kwanza, kufuatia kuachana na Xabi Alonso baada ya kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Barcelona kwenye fainali ya Supercopa de España. Uamuzi huo umefikiwa katika mazingira ya presha kubwa, huku uongozi wa klabu ukiongozwa na Rais Florentino Pérez ukisisitiza haja ya kurejesha uthabiti, mshikamano na matokeo yanayoendana na hadhi ya Los Blancos.
Alonso, aliyerithi mikoba ya Carlo Ancelotti kabla ya Kombe la Dunia la Klabu 2025, alikaa kwenye benchi la ufundi kwa takribani miezi saba, akisimamia jumla ya mechi 34. Hata hivyo, licha ya kuingia na sifa kubwa na matarajio makubwa, safari yake haikuwa laini. Taarifa kutoka ndani ya klabu zinaeleza kuwa kulikuwepo na matokeo yasiyoridhisha, hasa kwenye mechi kubwa, sambamba na tofauti za kimtazamo na baadhi ya wachezaji wakuu, hali iliyosababisha hali ya sintofahamu ndani ya kikosi.
Chanzo cha karibu na uongozi wa Madrid kimeeleza kuwa kipigo dhidi ya Barcelona kilikuwa tone la mwisho katika uamuzi wa kumwondoa Alonso. Ingawa timu ilikuwa ikionyesha vipindi vya uchezaji mzuri, ukosefu wa mwendelezo, mabadiliko ya mara kwa mara ya mfumo, pamoja na tetesi za kutoelewana kuhusu majukumu ya wachezaji, vilichangia kupungua kwa imani ya bodi. Perez na washauri wake waliamini kuwa kikosi kilihitaji sauti mpya yenye uwezo wa kuunganisha chumba cha kubadilishia nguo na kurejesha utambulisho wa Madrid.

Baada ya kuondoka kwa Alonso, Real Madrid imegeukia uso unaoufahamu vizuri utamaduni wa klabu Álvaro Arbeloa. Uteuzi huu unaonekana kuwa wa kimkakati kwa sababu kadhaa. Kwanza, Arbeloa ni zao la akademi ya Madrid na ni mchezaji wa zamani mwenye historia ndefu ndani ya klabu, jambo linalompa uelewa mpana wa presha, matarajio na falsafa ya Los Blancos. Pili, amejijengea uzoefu wa ukocha kwa ngazi za vijana, akionyesha uwezo wa kuibua vipaji na kusimamia nidhamu.
Arbeloa alijiunga na mfumo wa ukocha wa Madrid mwaka 2020 kama kocha wa Under-14, kabla ya kupanda ngazi hatua kwa hatua hadi kuchukua nafasi ya Raúl González kama kocha wa Castilla Mei mwaka jana. Ndani ya muda huo, amesifiwa kwa mbinu za kisasa, usimamizi mzuri wa wachezaji vijana na uwezo wa kujenga timu zenye ushindani. Haya yote yamemfanya Perez kumuona kama chaguo salama na la muda mrefu.
Kama mchezaji, Arbeloa alipitia akademi ya Madrid na kucheza mechi yake ya kwanza ya timu ya wakubwa Oktoba 2004. Aliondoka mwaka 2005 kabla ya kurejea tena mwaka 2009, akiitumikia klabu kwa miaka saba hadi 2016. Katika kipindi hicho, alicheza mechi 237 katika mashindano yote na kutwaa mataji makubwa yakiwemo LaLiga, Copa del Rey mara mbili, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili, Kombe la Dunia la Klabu na Super Cup. Rekodi hiyo inampa heshima kubwa miongoni mwa mashabiki na ndani ya chumba cha kubadilishia nguo.
Sababu nyingine iliyomvutia Perez ni mshikamano na uelewano wa Arbeloa na kizazi cha sasa cha wachezaji, pamoja na historia yake ya kucheza bega kwa bega na Alonso katika Liverpool na Real Madrid. Uongozi unaamini Arbeloa ana mawasiliano bora, nidhamu na uwezo wa kuunganisha wachezaji wakubwa na vijana kile ambacho kilionekana kupungua katika kipindi cha mwisho cha Alonso.
Arbeloa anaingia kazini wakati Madrid ipo nafasi ya pili kwenye LaLiga, ikiwa pointi nne nyuma ya Barcelona. Kibarua chake cha kwanza kitakuwa Jumatano dhidi ya Albacete katika Copa del Rey, mechi itakayokuwa kipimo cha awali cha falsafa yake na mwelekeo wa timu chini ya uongozi wake.
Kwa Perez, uteuzi wa Arbeloa ni ujumbe wazi kurejesha utulivu, utambulisho na ushindani. Mashabiki sasa wanasubiri kuona kama kocha huyu kijana ataweza kuhimili presha ya Santiago Bernabéu na kuiongoza Madrid kurejea kwenye njia ya ushindi haraka na kwa uthabiti.
