Azam Fc Wapata C.E.O Mpya

Klabu ya Azam Football Club imeingia katika ukurasa mpya wa mageuzi ya kiuongozi baada ya Bodi ya Wakurugenzi kutangaza rasmi kumteua Mhispania Octavi Anoro, mwenye umri wa miaka 42, kuwa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya wa klabu hiyo. Uteuzi huu unakuja kupitia mkataba wa miaka miwili unaotarajiwa kudumu hadi mwaka 2027, na kuashiria dira mpya ya maendeleo ndani ya moja ya vilabu vinavyoongoza katika soka la Tanzania.
Nafasi ya Mtendaji Mkuu ilikuwa wazi baada ya aliyekuwa akiishikilia, Abdulkarim Nurdin ‘Popat’, kupandishwa cheo na kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa klabu. Mabadiliko haya yanatajwa na wadau wa soka kama dalili ya utulivu wa kiutawala na mipango madhubuti ya muda mrefu, ambayo imekuwa ikifanywa na klabu hiyo inayojulikana kwa uwekezaji wake wa kitaaluma ndani na nje ya uwanja.
ANORO: MTALAAM WA KIMATAIFA ANAYEKUJA KUONGEZA NGUVU MPYA
Octavi Anoro anawasili Azam FC akiwa na mkoba mzito wa ujuzi, uzoefu na rekodi thabiti katika nyanja za maendeleo ya utawala, biashara ya michezo na uendeshaji wa klabu za mpira wa miguu katika kiwango cha kimataifa. Kutoka Hispania—nchi maarufu kwa historia ya soka lenye ubora wa kiufundi, mifumo imara ya kiutawala na falsafa ya kisasa ya maendeleo ya vipaji,Anoro anategemewa kuwa chachu muhimu katika kuinua hadhi ya Azam FC ndani ya soka la Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi, uteuzi wa Anoro unalenga kuimarisha uendeshaji wa klabu, kuongeza thamani ya kibiashara, kukuza mipango ya maendeleo ya vijana na kuhakikisha klabu inapiga hatua katika ushindani wa ndani na kimataifa. Uwepo wake unatarajiwa kuleta maboresho katika maeneo ya usimamizi wa rasilimali watu, masoko, miundombinu, pamoja na uimarishaji wa mifumo ya kiutendaji inayokidhi viwango vya kisasa.
RASHA SEIF: MCHAMBUZI WA KISASA MWENYE ELIMU NA UJUZI WA KIMATAIFA
Sambamba na uteuzi wa Anoro, Bodi pia imemteua Rashid Seif Mohamed kuwa Msaidizi wa Mtendaji Mkuu (Assistant CEO). Rashid anakuja na elimu ya juu katika uongozi wa michezo, akiwa mhitimu wa Shahada ya Umahiri (Master’s in Sports Management) pamoja na Leseni ya Pili ya Ukocha kutoka Chama cha Soka cha England (FA), ambayo ni moja ya taasisi zenye viwango vya juu zaidi duniani.
Kupitia elimu na mafunzo yake ya kimataifa, Rashid anatarajiwa kuwa kiungo muhimu katika kusimamia utekelezaji wa mikakati ya muda mrefu ya klabu, huku akisaidia kujenga mazingira bora ya kiutawala, kiushindani na kitaaluma kwa wachezaji, benchi la ufundi na watendaji wa klabu.
AZAM FC YAPIGA HATUA KWENYE MAGEUZI YA UONGOZI
Kwa miaka kadhaa sasa, Azam FC imeendelea kujipambanua kama mojawapo ya vilabu vinavyoendeshwa kitaaluma zaidi nchini, ikiwa na viwango vya juu katika usimamizi, miundombinu ya kisasa kama Azam Complex, pamoja na sera za kuendeleza vipaji kupitia kituo cha vijana. Uteuzi huu mpya unaongeza nguvu katika dhamira ya klabu kubaki kwenye mstari wa ubora na ushindani barani Afrika.
Ni wazi kuwa klabu hiyo inalenga kujijenga si tu kama mshindani wa kutwaa makombe, bali pia kama taasisi ya kisasa yenye misingi imara ya kiutawala na biashara mambo ambayo ndio msingi wa mafanikio ya vilabu vikubwa duniani.
Wadadisi wa soka wanaamini kuwa ujio wa Anoro na Rashid utafungua ukurasa mpya katika safari ya Azam FC, safari yenye matumaini, mikakati kabambe na mapinduzi chanya yatakayoiongezea klabu nguvu ya kiushindani katika misimu ya mbele.
Kwa ujumla, hatua hizi za Bodi zinaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa klabu kuhakikisha ustawi wa muda mrefu, ukuaji wa kimkakati, na kuendelea kuweka alama katika maendeleo ya utawala wa michezo nchini Tanzania.



