Marcio Maximo Akalia Kuti Kavu Kmc Fc

Screenshot 20251117 121731 Instagram

Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Madenyeka, ameweka wazi kuwa mustakabali wa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbrazil Marcio Maximo, bado haujafikia tamati licha ya mwenendo mbovu unaoendelea kuitesa timu hiyo kwenye Ligi Kuu Bara. Akizungumza kwa kifupi lakini kwa msisitizo, Madenyeka amesema uongozi wa KMC unafahamu presha iliyopo kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka, lakini hawapo tayari kufanya maamuzi ya haraka bila kufuata utaratibu na muda sahihi.Marcio Maximo Akalia Kuti Kavu Kmc Fc-www.sportsleo.co.tz

Akizungumza na Sportsleobongo, Madenyeka amesema hakuna kiongozi ndani ya klabu hiyo anayeridhishwa na kiwango cha timu kwa sasa, huku akisisitiza kuwa uongozi nao unahisi uchungu ule ule ambao mashabiki wanaupata kila wanapoona matokeo mabaya yanayojirudia kila wiki. Hata hivyo, ameeleza kuwa suala la kuachana na Maximo ni nyeti na linahitaji maamuzi ya kina, si kwa presha wala jazba, bali kwa kuangalia maslahi ya muda mrefu ya klabu.

“Hatuwezi kukurupuka. Tunajua kuna shinikizo, tunajua timu haipo vizuri, lakini lazima tufanye maamuzi kwa wakati sahihi. Tukiwa na uhakika, tutachukua hatua,” amesema Madenyeka kwa utulivu.

Madenyeka, ambaye hivi karibuni alichukua nafasi ya Daniel Mwakasungula aliyemaliza muda wake, amesema hawezi kukubali kuona KMC ikishuka daraja ikiwa mikononi mwake. Amedai mipango ya kuinusuru timu hiyo ipo, na tayari ameanza kufanya vikao maalum na benchi la ufundi pamoja na wachezaji ili kubaini mahali palipo kasoro na namna ya kurejesha uhai wa kikosi hicho.

Marcio Maximo Akalia Kuti Kavu Kmc Fc-www.sportsleo.co.tz

Pamoja na kutia matumaini, taarifa zinaeleza kuwa Maximo yupo kwenye hatua za mwisho za kuachana na klabu hiyo. Kilichobaki, kwa mujibu wa taarifa zetu, ni kumalizia mazungumzo ya kifedha, ikiwemo malipo ya kuvunja mkataba wake ili aweze kuondoka kwa taratibu bila mgogoro. Inaelezwa uongozi hauko tayari kuendelea kumlipa kocha huyo bila kupata matokeo uwanjani, wakati timu ikiendelea kuzama kwenye nafasi ya hatari.

Takwimu zinaendelea kumweka Maximo kwenye wakati mgumu tangu ajiunge na kikosi hicho mwanzoni mwa msimu huu, KMC imeshinda mechi moja tu ya Ligi Kuu. Mechi nyingine sita, tano amepoteza mfululizo huku akiruhusu mabao 10 na kufunga mabao mawili pekee. Hali hiyo imesababisha timu iburuze mkia kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi tatu pekee, hali ambayo haikubaliki kwa mashabiki wala kwa uongozi mpya.

Kwa wale wanaofuatilia soka la Tanzania, jina la Marcio Maximo halihitaji utambulisho mrefu. Hii ni mara ya tatu kocha huyo kutua nchini kufundisha, baada ya kufanya kazi kubwa akiwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars kuanzia mwaka 2006 hadi 2010 kipindi ambacho alijizolea umaarufu mkubwa kwa kukisuka kikosi cha vijana na kukipa nidhamu mpya. Baadaye aliinoa Yanga mwaka 2014, akiacha kumbukumbu ya mabadiliko mbalimbali ya kiufundi ndani ya klabu hiyo.

Kumbukumbu nzuri zaidi kwenye macho ya Watanzania, bila shaka, ni ile ya mwaka 2009 alipokuwa kocha wa kwanza kuipeleka Taifa Stars kwenye fainali za CHAN nchini Ivory Coast mashindano ya kwanza kabisa ya kimataifa ambayo Stars ilishiriki kupitia wachezaji wa ndani pekee. Maximo amerudi nchini akiamini ataendeleza rekodi hizo, lakini safari yake mpya ndani ya KMC inaonekana kuwa tofauti kabisa na alivyotarajia.

Kwa sasa macho yote yako kwa uongozi wa KMC kuona ni lini watatoa tamko rasmi kuhusu hatma ya kocha huyo. Mashabiki wao wanaendelea kushika pumzi, wakitumaini maamuzi ya busara yatakayoirudisha timu kwenye mstari na kuinusuru isiende kushuka daraja msimu huu ambao umekuwa mgumu zaidi kuliko ilivyowahi kutokea.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks