Simba Sc,Kapombe Waangukia Pua Caf

Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetaja majina ya klabu tatu zilizofanikiwa kutinga hatua ya mwisho ya kuwania tuzo ya Timu Bora ya Mwaka ya Wanaume (CAF Awards 2025 – Club of the Year Finalists), na kama ilivyotarajiwa, mabingwa na wababe wa Afrika kutoka ukanda wa Kaskazini na Kusini wameendelea kutikisa orodha hiyo.
Kwa mujibu wa CAF, klabu zilizofanikiwa kupenya hadi hatua ya mwisho ni Pyramids FC ya Misri, RS Berkane ya Morocco na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Hizi ndizo timu ambazo zilionesha ubora mkubwa katika michuano ya CAF msimu uliopita hivyo kupewa nafasi ya kuwania taji hilo kubwa linalowahusu mabingwa wa ngazi ya klabu.
Pyramids imepata heshima hiyo baada ya kufanya kazi kubwa kwenye Kombe la Shirikisho pamoja na Ligi ya Misri, wakati RS Berkane ikitumia uzoefu wake mkubwa kwenye michuano ya CAF kuingia kwenye orodha hiyo kwa mara nyingine tena. Kwa upande wa wababe wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns, mafanikio yao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na utawala wao barani Afrika umeendelea kuwapa nafasi kubwa katika tuzo kama hizi.
Wakati klabu zikisubiri mwamuzi wa mwisho, macho ya mashabiki wa Tanzania yalikuwa kwa beki mahiri wa Simba SC, Shomari Kapombe, ambaye alikuwa katika orodha ya wanaowania tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika (Best African Player in Interclub Competitions). Hata hivyo, Kapombe ameondolewa katika hatua ya mwisho baada ya ushindani kuwa mkali zaidi, na kubakiwa mastaa watatu tu akiwemo aliyewahi kuwika VPL, Fiston Mayele wa Pyramids.
Awali Kapombe alikuwa anachuana na wachezaji 10 ambao wamekuwa na misimu mizuri zaidi barani Afrika akiwamo Ismael Belkacemi wa Al Ahli Tripoli, kiungo wa Pyramids Blati Touré, beki hatari mwenye historia ndefu na RS Berkane Issoufou Dayo, mshambuliaji nyota Fiston Mayele, pamoja na mastaa wengine kama Ahmed Samy, Emam Ashour, Ibrahim Adel, Mohamed Hrimat, Mohamed Chibi na Oussama Lamlioui.
Kutolewa kwa Kapombe kumewakasirisha baadhi ya mashabiki wa nchini, hasa ukizingatia kiwango chake ndani ya Simba na timu ya taifa, lakini ukweli ni kwamba ushindani ulikuwa mkubwa mno msimu huu.
Wakati Kapombe akifungashiwa virago, habari njema imekuja kwa upande wa klabu ya Yanga kupitia kwa mshambuliaji chipukizi anayeendelea kupaa, Clement Francis Mzize, ambaye ameingia katika orodha ya awali ya Tuzo ya Bao Bora Afrika.
Mzize amewekwa kwenye orodha hiyo kutokana na bao lake tamu alilofunga Januari 4 mwaka jana katika ushindi wa 3-1 dhidi ya TP Mazembe kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Bao hilo ambalo lilikuwa la kusawazisha dakika ya 33 liliibua shangwe kubwa jukwaani, baada ya TP Mazembe kutangulia kupata bao la mapema kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na kipa wao, Aliouane Badara Faty, dakika ya 16. Uhodari wa Mzize katika nafasi ya ushambuliaji ulijidhihirisha siku hiyo, kwani hakuishia hapo.
Alifunga tena dakika ya 60 akihitimisha ‘usiku wake wa dhahabu’, ambapo kabla yake kiungo hatari wa Yanga kipindi hicho, Stephane Aziz Ki, aliifungia timu hiyo bao la pili dakika ya 56. Hilo lilikuwa moja ya michezo iliyothibitisha kuwa Mzize si tu chipukizi bali nyota anayekua kwa kasi barani Afrika.
Kwa mashabiki wa Yanga, kitendo cha kijana wao kuingia kwenye orodha ya CAF ni ishara kuwa klabu inazidi kutambulika kimataifa. Kwa upande mwingine, kitendo cha Kapombe kutolewa kwenye mchujo wa mwisho kinarejesha mjadala kuhusu nafasi ya wachezaji wa Tanzania kwenye majukwaa makubwa ya CAF.
Hivi sasa macho yote yameelekezwa kwenye sherehe za mwisho za CAF Awards 2025. Nani atanyakua tuzo? Je, Mzize ataendelea kuwepo hadi hatua ya mwisho? Mashabiki wanasubiri kwa hamu, huku mastaa wa Afrika wakiendelea kupambana kuandika historia mpya.


