Barker Rasmi Aanza Kazi Simba Sc,Matola Amkaribisha

www.sportsleo.co.tz

Kocha Mkuu mpya wa Klabu ya Simba, Steve Barker, ameanza rasmi majukumu yake baada ya kukutana na kukaribishwa na kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Suleiman Matola, katika kikao cha kwanza kilichofanyika jana kwa lengo la kumtambulisha kocha huyo kwenye mazingira ya klabu na maandalizi ya kazi inayomsubiri.

Barker aliwasili akiwa ameongozana na makocha wake wasaidizi wawili, akiwemo Deen ambaye ni mchambuzi wa video, na wote walipokelewa na Matola ambaye kwa sasa anatarajiwa kubaki benchi la ufundi kama kocha msaidizi namba mbili chini ya uongozi wa Barker.

Katika mazungumzo yao ya awali, Matola alimpa Barker muhtasari wa hali ya kikosi, mazingira ya klabu pamoja na ratiba ya karibu ya mashindano, huku mkutano huo ukielezwa kuwa wa kirafiki lakini wenye malengo ya kitaalamu kwa mustakabali wa Simba.

MATOLA AWAPOKEA BARKER NA WENZAKE ✅Kocha mkuu wa klabu ya Simba akiwa ameongozana na makocha wa 2

Chanzo cha ndani ya klabu hiyo kiliiambia Sportsleo kuwa kikao hicho kililenga zaidi kumpa Barker picha ya jumla ya Simba, ikiwemo mwenendo wa wachezaji, changamoto zilizokuwepo msimu uliopita na matarajio ya uongozi pamoja na mashabiki wa timu hiyo.

“Matola amefanya kazi ya awali kumpa Barker mwanga. Amezungumza naye kwa kina kuhusu kikosi, aina ya wachezaji waliopo na hata maeneo ambayo yanahitaji maboresho. Pia amemtambulisha kwa wasaidizi wake ili kuanza kujenga maelewano mapema,” kilisema chanzo hicho.

Steve Barker anatarajiwa kuanza rasmi kusimamia mazoezi ya Simba kuanzia kesho, ikiwa ni maandalizi ya kuelekea michuano ya Mapinduzi Cup, mashindano ambayo Simba ni miongoni mwa washiriki wakuu. Mashindano hayo yanatazamwa kama kipimo cha awali kwa Barker kuanza kuionyesha falsafa yake ya soka ndani ya kikosi hicho.

Kwa mujibu wa ratiba ya klabu, Barker atapewa muda mfupi kuijenga timu kabla ya Mapinduzi, huku akilazimika kufanya tathmini ya haraka ya wachezaji waliopo na mfumo anaotaka kuutumia, jambo linaloongeza presha kwa kocha huyo raia wa Afrika Kusini.

Imeelezwa kuwa Barker pia anategemewa kukabidhiwa ripoti ya kina ya kikosi kutoka kwa Matola, ikijumuisha taarifa za mwenendo wa kila mchezaji, kiwango chake, nidhamu, majeruhi na nafasi anazocheza. Ripoti hiyo inatarajiwa kuwa nyenzo muhimu kwa kocha huyo mpya kupanga mipango yake ya muda mfupi na mrefu.

Mbali na hilo, Barker atakabidhiwa pia ripoti za makocha waliopita, ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa klabu hiyo kuhakikisha mwendelezo wa taarifa na kuepuka kuanza upya kila mara. Ripoti hizo zinatajwa kuwa zitamsaidia Barker kuelewa ni wapi Simba ilikwama na ni maeneo gani yanahitaji mabadiliko ya haraka.

“Lengo ni kumpa Barker picha kamili ya Simba. Uongozi unataka aanze kazi akiwa na taarifa zote muhimu ili aweze kuisuka Simba mpya yenye ushindani mkubwa ndani na nje ya nchi,” kiliongeza chanzo hicho.

Kwa upande wake, Suleiman Matola anaelezwa kuwa tayari kwa jukumu lake jipya kama kocha msaidizi namba mbili, akisisitiza ushirikiano na Barker pamoja na benchi lote la ufundi kwa maslahi ya timu. Matola, ambaye amewahi kuinoa Simba katika vipindi tofauti, ana uzoefu mkubwa wa mazingira ya klabu hiyo na anatajwa kuwa rasilimali muhimu kwa Barker.

Mashabiki wa Simba wana matarajio makubwa kwa Barker, wakiamini kuwa ujio wake utarejesha makali ya timu hiyo baada ya misimu ya changamoto. Hata hivyo, wachambuzi wa soka wanaonya kuwa kocha huyo atahitaji muda, subira na sapoti ya kila mmoja ili kufanikisha malengo yake.

Michuano ya Mapinduzi inatajwa kuwa mwanzo wa safari mpya ya Simba chini ya Barker, safari ambayo itapimwa kwa matokeo, mtindo wa uchezaji na uwezo wa timu kurejesha heshima yake katika mashindano ya ndani na ya kimataifa.

Kadri siku zinavyosonga, macho ya mashabiki na wadau wa soka yataendelea kumtazama Barker kuona ni namna gani atakavyoanza kuisuka Simba mpya yenye tishio, huku matumaini yakiwa makubwa kuwa zama mpya zimeanza Msimbazi.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks