Chalamila Atimiza Ahadi: Yakoub Suleiman Akabidhiwa Gari Aina Ya Crown

Screenshot 20250922 214424 Instagram

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila, ameendelea kuthibitisha kuwa yeye ni kiongozi wa vitendo na si maneno, baada ya kutimiza ahadi yake ya kumpa gari golikipa wa Taifa Stars, Yakoub Suleiman.

Ahadi hiyo aliitoa wakati wa fainali za michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), ambapo Taifa Stars licha ya kutolewa hatua ya robo fainali na Morocco, kipa huyo chipukizi aliibua taswira mpya ya ujasiri na nidhamu ya juu katika lango la Tanzania.

Chalamila Atimiza Ahadi: Yakpub Suleiman Akabidhiwa Gari Aina Ya Crown-Sportsleo.co.tz

Tukio hilo la kukabidhi gari aina ya Toyota Crown lilifanyika leo katika ofisi za Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, likihudhuriwa na waandishi wa habari, viongozi wa michezo pamoja na wadau wa soka.

Yakoub Suleiman, ambaye hivi sasa amejiunga na mabingwa wa kihistoria wa Tanzania, Simba SC, akitokea JKT Tanzania, alionekana mwenye furaha na mshangao mkubwa huku akishukuru kwa heshima hiyo kutoka kwa mkuu wa mkoa.

Akizungumza mara baada ya kumkabidhi funguo za gari hilo, Mh. Chalamila alisema “Ahadi ni deni. Niliwaahidi Watanzania na huyu kijana kuwa nitamtunuku gari kwa ujasiri wake aliouonyesha pale CHAN. Licha ya Stars kutolewa, lakini heshima yake langoni na moyo wake wa kizalendo ulitupa matumaini mapya. Leo nimesimama mbele yenu kutimiza nilichosema, na nataka vijana wengine wajifunze kuwa nidhamu, kujituma na uzalendo hulipa.”

Yakoub, kwa upande wake, hakuficha hisia zake. Alisema huu ni mwanzo mpya katika safari yake ya soka, huku akisisitiza kuwa zawadi hiyo ni chachu ya kuendelea kupigania bendera ya Tanzania ndani na nje ya uwanja.

“Kwa kweli sijawahi kufikiria kama ningepata zawadi kubwa kama hii mapema katika maisha yangu ya soka. Namshukuru sana Mheshimiwa Chalamila kwa upendo huu. Nitajituma zaidi Simba SC na Taifa Stars ili kuonyesha kuwa vijana wa kitanzania tunaweza.”

Zawadi hiyo imepokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wa soka nchini, wengi wakisema kitendo cha Chalamila kinaonyesha mfano wa kiongozi anayejali na kuthamini vipaji vya vijana. Katika mitandao ya kijamii, baadhi ya mashabiki waliandika kuwa hatua hiyo itawatia moyo wachezaji wengine kujituma zaidi wanapovaa jezi ya taifa.

Kukabidhiwa gari hili pia kunakuja wakati mzuri kwa Yakoub, ambaye hivi sasa anaingia rasmi kwenye ukurasa mpya wa maisha yake ndani ya kikosi cha Simba SC.

Ujio wake klabuni hapo unatarajiwa kuongeza ushindani wa nafasi ya mlinda mlango, huku akichukuliwa kama mrithi wa muda mrefu kutokana na umri wake mdogo na uwezo mkubwa alioonyesha katika CHAN.

Kwa hakika, tukio hili limeandika historia si tu katika maisha ya Yakoub Suleiman, bali pia katika uhusiano wa michezo na uongozi wa kisiasa nchini. Wengi wanakiri kuwa zawadi hii ni zaidi ya gari; ni ujumbe kuwa juhudi, nidhamu na uzalendo huwa havipotei bure.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks