Hali Tete Sakata la Usajili wa Mohamed Hussein

Hali Tete sakata la usajili wa Mohamed Hussein ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya beki huyo wa kushoto kumaliza mkataba wake wa miaka miwili katika klabu ya Simba Sc aliousaini misimu miwili iliyopita na sasa mchezaji huyo anaangalia aina ya ofa alizonazo ikiwemo ya waajiri wake hao wa mwanzoni.
Mabosi wa Simba sc walijaribu mara kadhaa kufanya mazungumzo na beki huyo kabla ya msimu kumalizika lakini hawakufikia muafaka kama ilivyo kwa mazungumzo ya sasa ambapo mchezaji huyo anahitaji dau la usajili kiasi cha shilingi milioni mia nne sambamba na mshahara wa shilingi milioni kumi na tano kwa mwezi.

Hata hivyo mazungumzo hayo hayajafikia muafaka ambapo mabosi wa klabu hiyo wanataka mchezaji huyo ashushe kidogo dau la usajili huku pia wakikubaliana basi moja kwa moja ripoti itafika kwa Mohamed Dewji kwa ajili ya kukamilisha dili hilo.
Wasiwasi mkubwa umetanda kwa mashabiki wa Simba sc kufuatia kauli ya Meneja wa Idara ya habari na mawasiliano wa klabu hiyo Ahmed Ally kusema kwa mashabiki wa klabu hiyo wajiandae kwa lolote kuhusu hatma ya beki huyo aliyedumu takribani miaka kumi klabuni hapo.
“Ni kweli Mohammed Hussein amemaliza mkataba wake na juhudi zilifanyika kuongeza mkataba ila bado hajasaini, hivyo lazima wana Simba tuwe tayari kupokea chochote ambacho viongozi wataamua kuhusiana na Tshabalala”Alisema katika hali ya unyonge msemaji huyo mwenye mbwembwe nchini.
Pia mbali na hilo Ahmed Ally aligusia kuhusu zoezi la usajili wa mastaa wapya kikosini humo huku tetesi za kukaribia kumsajili kiungo Mousa Balla Conte kutoka Cs Sfaxien ya nchini Tunisia.
“Viongozi wamesambaa nchi mbalimbali za Afrika kwa ajili ya kumalizana na wachezaji tuwalete kwenye klabu yetu, kwa mara ya kwanza huu ndio usajili ambao tunatumia asilimia 100 ya pendekezo la benchi la ufundi”.Alisema huku akiendelea kusema kuwa “Mwaka huu nitawaacha watu waone wenyewe aina ya mali ambazo tutazishusha.Safari hii, sitaongea sana”.Alimalizia kusema msemaji huyo
Simba Sc msimu huu inapaswa kuboresha kikosi chake ili iweze kurejesha makali yake kutokana na kukaa miaka minne bila taji lolote huku wakifungwa mara kwa mara na watani zao wa jadi Yanga sc.
