Kilele Cha Wiki Ya Wananchi: Yanga Day Ya Kihistoria Dsm

Screenshot 20250913 134530 Instagram

Jana, Septemba 12, jiji la Dar es Salaam lilishuhudia shamrashamra kubwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, wakati Klabu ya Yanga SC ilipofanya kilele cha Wiki ya Wananchi, tukio ambalo kwa mara nyingine limeandika historia ya soka la Tanzania.

FB IMG 1757760118159

Yanga Day, kama ilivyozoeleka, si tu tamasha la michezo bali ni sherehe ya kijamii na kiutamaduni inayounganisha mashabiki, wasanii, wachezaji na wadau wa michezo wote nchini Tanzania ambapo siku hiyo huwa ni burudani kuanzia asubuhi mpaka jioni.

Kuanzia asubuhi, mitaa ya jiji ilikuwa kwenye hekaheka ya kijani na njano, rangi ambazo zilipamba anga lote la Dar,Mashabiki walijitokeza kwa wingi wakiwa na jezi mpya za msimu, nyimbo na kelele za vifijo na vigelegele zikitawala.

FB IMG 1757760132857

Wenyeji wa tamasha hilo, Yanga SC, walihakikisha kila shabiki aliyefika uwanjani anapata burudani isiyo na kifani, ikiwemo muziki,Vichekesho,burudani na hatimaye utambulisho rasmi wa wachezaji wapya waliowasajili kwa msimu wa 2025/26.

Sehemu ya kwanza ya sherehe ilianza na maonyesho ya wasanii pamoja na michezo ya kirafiki ya soka baina ya Menejimenti ya Yanga sc dhidi ya wasanii wa maigizo ambapo menejimenti ya Yanga Sc ilipata ushindi wa mabao 3-0.

Kisha burudani za wasanii kama Dogo Paten na D voice waliotikisa jukwaa na kufanya mashabiki wasahau hata joto la jiji la Dar. Mashabiki waliimba kwa nguvu, wakicheza sambamba na wasanii wao pendwa, hali iliyoonesha jinsi soka na muziki vinavyounganisha jamii kwa namna ya kipekee.

Kilele cha sherehe hiyo kilikuwa ni utambulisho wa mastaa wapya wa Yanga uliiongozwa na Haji Manara ambaye aliwaita Wachezaji kuingia uwanjani mmoja baada ya mwingine kwa mbwembwe na sifa kibao ambapo mashabiki walilipuka kwa shangwe hasa utambulisho wa Pacome Zouzoua na Moussa Balla Conte.

Screenshot 20250913 134415 Instagram

Usajili mpya wa timu hiyo umeleta matumaini makubwa kwa mashabiki wa Wananchi, kwani unahusisha wachezaji wenye uzoefu wa kimataifa pamoja na nyota chipukizi wanaoonekana kuleta nguvu mpya kikosini. Wachezaji kama Lassine Kouma, Andy Boyeli na Celestine Ecua ambapo walipokanyaga nyasi za Benjamin Mkapa, kila mmoja alipokewa kwa mbwembwe na vigelegele vya kipekee.

Msanii Zuhura Othman Soud maarufu kama Zuchu alikonga nyayo za mashabiki wa klabu hiyo kwa kutoa burudani safi kabisa uwanjani hapo akiimba kwa mpangilio mzuri wenye sauti ya kuvutia huku akibadilika kila mara katika kulitawala jukwaa.

Screenshot 20250913 134658 Instagram

Baada ya shamrashamra hizo, Yanga SC walicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Bandari FC ya Kenya walioibuka na ushindiwa1-0 lilipotikana mapema dakika ya 2 ya mchezo Ingawa ulikuwa mchezo wa maandalizi, umati wa mashabiki ulishuhudia mpira wa kiwango cha juu. Yanga walionekana kujiandaa kwa msimu mpya, huku safu ya ulinzi na kiungo ikionekana imara, na washambuliaji wakionesha dalili za moto ujao.

Mchezo huo ulihitimisha siku kwa kutoa burudani ya kweli, huku mashabiki wakionekana kuridhishwa na mwelekeo wa timu yao kipenzi.

Lakini upekee wa Yanga Day ya mwaka huu haukuishia tu kwenye muziki, wachezaji na mashabiki. Tukio kubwa lililovuta hisia za wengi ni wakati serikali ilipokabidhi hati ya uwanja kwa klabu ya Yanga SC. Hatua hiyo imeweka msingi mpya wa maendeleo, kwani sasa Yanga itaanza rasmi mchakato wa kujenga uwanja wao wa kisasa, jambo ambalo litaongeza hadhi ya klabu na kuchochea maendeleo ya soka nchini.

Mashabiki walilipuka kwa shangwe mara hati hiyo ilipokabidhiwa na waziri wa Ardhi Deogratius Ndejembi kwa Rais wa Yanga sc Eng.Hersi Said wakijua kuwa ndoto ya kuwa na uwanja wa nyumbani wa kisasa eneo la Jangwani ipo karibu kutimia.

Screenshot 20250913 134600 Instagram

Kwa hakika, Yanga Day ya mwaka huu imeacha alama ya kudumu. Mashabiki walipata burudani ya muziki na mpira, wachezaji wapya walionekana wakiwa tayari kupigania jezi ya kijani na njano, na historia mpya iliandikwa kupitia hati ya ujenzi wa uwanja.

Tukio hili limeonesha kwa mara nyingine kuwa Yanga SC si klabu ya mpira pekee, bali ni taasisi kubwa ya kijamii inayogusa maisha ya Watanzania kwa upana.

Kwa jumla, tamasha la jana limezidi kuthibitisha kuwa Yanga SC ni timu yenye mashabiki wa kipekee, yenye mipango ya muda mrefu, na yenye dira ya kufanikisha ndoto kubwa za kitaifa na kimataifa. Yanga Day 2025 itabaki kwenye kumbukumbu kama moja ya matamasha bora zaidi kuwahi kufanyika nchini.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks