Mzize Atwaa Tuzo Caf

584011746 18181290115358691 376411324645096929 n

Mshambuliaji matata wa Yanga SC, Clement Mzize, ameandika historia mpya kwenye ramani ya soka la Afrika baada ya kutangazwa mshindi wa Tuzo ya Goli Bora la Mwaka (CAF Goal of the Season 2025) katika hafla ya kifahari ya Tuzo za CAF 2025 zilizofanyika mjini Rabat, Morocco.

Hii ni mara ya kwanza kwa mchezaji mzawa wa Tanzania kushinda tuzo hiyo kubwa, jambo lililowafanya mashabiki wa Yanga Sc na Watanzania kwa ujumla kusherehekea kama ushindi wa taifa.

Mzize Atwaa Tuzo Caf-www.sportsleo.co.tz

Mzize ametwaa tuzo hiyo kupitia bao lake la shuti kali la umbali wa zaidi ya mita 25 alilolifunga dhidi ya TP Mazembe katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita  bao ambalo lilitikisa mitandao, likawa gumzo barani Afrika na hata kuvutia wataalam wa soka duniani walioliona kama “risasi ya dhahabu”.

Hata hivyo, licha ya kuibuka shujaa wa Afrika, Mzize hakuweza kusafiri kwenda kupokea tuzo hiyo kutokana na kufanyiwa upasuaji wa goti wiki kadhaa zilizopita ambapo mujibu wa madaktari wake, safari ya anga kwa umbali mrefu ingehatarisha mchakato wa kupona, hivyo mshambuliaji huyo alibaki jijini Dar es Salaam akitazama hafla hiyo kupitia runinga. Mashabiki walionekana kuguswa na hali yake, lakini CAF waliweka rekodi maalum ya kumpongeza kwa kipaji na kazi aliyoweka msimu uliopita.

Mzize Atwaa Tuzo Caf-www.sportsleo.co.tz

“Nawashukuru CAF kwa kunipa tuzo hii…! Naamini itakwenda kuongeza hamasa zaidi na tuzo hii itaniongezea thamani zaidi na nawashukuru wachezaji wenzangu kwa kuniunga mkono na Nawashukuru watu wote.Alisema mchezaji Clement Mzize katika kipande cha video alichorekodiwa na kuchezwa ukumbini hapo.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa na mabingwa wa zamani wa soka barani Afrika, Asamoah Gyan wa Ghana na Manucho wa Angola, mastaa waliotikisa Ligi ya Mabingwa na mashindano ya mataifa ya Afrika katika miaka ya 2010. Wote wawili walimsifia Mzize wakisema goli lake lilikuwa na “ubunifu, nguvu na ubora wa kimataifa”, wakimtabiria mustakabali mkubwa kwenye soka la kufikia viwango vya juu barani na duniani.

Wakati Mzize akiendelea kupokea pongezi kutoka kona zote za bara, upande wa Yanga SC nao uliendelea kula presha kutoka kwa timu zinazotaka kumnasa mshambuliaji huyo. Kwa msimu mzima uliopita, klabu kubwa kutoka Mashariki ya Kati zimekuwa zikimfuatilia kwa karibu, huku vigogo wa soka la Libya Al Ahly Tripoli  wakiripotiwa kutuma ofa nono inayokadiriwa kufika bilioni tano za Kitanzania mwanzoni mwa msimu huu.

Hata hivyo, mabosi wa Yanga SC hawakuwa tayari kuachia huduma ya Mzize kirahisi. Vyanzo vya ndani ya klabu vilidokeza kuwa uongozi wa Yanga uliamua “kuweka ngumu” kwa madai kuwa thamani ya Mzize inaendelea kupanda, hasa kutokana na umri wake mdogo, kasi yake, uwezo wa kufunga katika mechi kubwa na kivutio anachotoa kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Uongozi wa Yanga ulikaa kwa muda mrefu mezani kuchambua ofa hiyo, lakini hatimaye wakaamua kumbakiza kutokana na mipango ya muda mrefu ya klabu, ikiwa pamoja na malengo yao ya kufanya vizuri zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Inaelezwa kuwa sababu nyingine ya klabu “kufunga mlango” ni kutokana na imani kuwa Mzize anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji watakaouzwa kwa dau kubwa zaidi katika historia ya Yanga au hata Tanzania.

Kwa sasa, Yanga SC wanasema wanajivunia mafanikio ya Mzize, wakisisitiza kuwa tuzo hiyo ni ushahidi wa uwekezaji wao katika vijana na nidhamu ya wachezaji wao. Kwenye mitandao ya kijamii, mashabiki wamemiminika kumpongeza huku wakileta tambo mbalimbali za kishabiki

Kwa upande wa mashabiki wa soka nchini, wengi wamesema ushindi wa Mzize ni ishara ya kuamka kwa vipaji vya Tanzania na kielelezo cha safari mpya ya soka la Bongo kusikika barani Afrika. Wengine walisema kuwa goli lake limeweka alama ambayo itakumbukwa kama ilivyokuwa bao la Pape Osmane Sakho wa Simba Sc  miaka ya nyuma lakini safari hii, limekuja na tuzo ya CAF.

Kwa ujumla, tuzo hii imemweka Mzize katika orodha ya wachezaji wanaoibukia kwa kasi kubwa barani Afrika. Huku akiendelea na matibabu, mashabiki wa Yanga na Taifa Stars wanaamini kwamba akiwa fiti msimu ujao, Mzize anaweza kuwa mchezaji muhimu zaidi kwenye mashindano ya kimataifa,Na kwa namna alivyoshinda mioyo ya mashabiki, inaonekana safari yake ya mafanikio ndiyo kwanza imeanza.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks