Nigeria Yatinga 16 Bora Afcon

Teamwork πŸ‡³πŸ‡¬ 1 1

Nigeria imefanikiwa kunusurika katika dakika za lala salama baada ya ushindani mkali kutoka Tunisia na hatimaye kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo uliochezwa usiku wa Jumamosi jijini Fez, Morocco. Ushindi huo umeifanya Nigeria kuwa timu ya pili kufuzu hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 yanayodhaminiwa na TotalEnergies.

Katika mchezo huo uliokuwa wa mwisho kati ya michezo minne mikali iliyochezwa nchini Morocco, Super Eagles walionekana kuwa mbele kwa kiwango kikubwa baada ya kuongoza kwa mabao 3-0, hali iliyowafanya mashabiki wao kuamini ushindi mwepesi. Hata hivyo, Tunisia walionyesha roho ya mapambano na kurejea kwa kishindo katika robo ya mwisho ya mchezo, jambo lililoufanya mchezo huo kuwa wa presha kubwa hadi dakika ya mwisho.

Mabao ya Montassar Talbi na Ali Abdi yaliipa Tunisia matumaini mapya, lakini Nigeria walionyesha ukomavu na nidhamu ya hali ya juu kulinda ushindi huo muhimu ambao umehakikisha wanatinga hatua ya mtoano mapema.

Nyota wa Nigeria, Ademola Lookman, alikuwa mhimili mkubwa wa ushindi huo baada ya kuonyesha kiwango cha juu kwa kufunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao. Kikosi cha kocha Eric Chelle kilianza kwa kasi, kikitawala eneo la kati na kutumia vyema mipira ya pembeni.

naija

Dakika moja kabla ya mapumziko, Lookman alitumia ustadi wake kupeleka mpira wa krosi wa uhakika kutoka upande wa kushoto, akimpata Victor Osimhen ambaye aliruka juu kwa nguvu na kupiga kichwa kilichotikisa nyavu za Tunisia, bao lililoamsha shangwe kubwa kwa mashabiki wa Nigeria.

Osimhen alikuwa tishio muda wote kupitia mipira ya juu, ambapo mapema alikuwa amejaribu bahati yake kwa vichwa viwili vilivyopita juu ya lango kwa tofauti ndogo sana.

Nigeria waliendelea na kasi ileile kipindi cha pili na hawakupoteza muda kuongeza bao la pili. Dakika nne tu baada ya kuanza tena, nahodha Wilfred Ndidi alionyesha ubora wake wa kuruka juu kwa kupiga kichwa safi kutoka kwenye kona iliyopigwa tena na Lookman, na kuifanya Nigeria iongoze kwa mabao 2-0.

Teamwork πŸ‡³πŸ‡¬

Mchezaji Bora wa Afrika wa CAF kwa mwaka 2024, Ademola Lookman, alikamilisha onyesho lake la kiwango cha juu dakika ya 66 kwa kufunga bao la tatu. Baada ya pasi safi kutoka kwa Osimhen, Lookman alipiga shuti kali la mguu wa kushoto akiwa ndani ya eneo la hatari na kuupiga mpira wavuni, bao lililoonekana kuhitimisha matumaini ya Tunisia.

Hata hivyo, Carthage Eagles hawakukata tamaa. Dakika ya 75, Montassar Talbi alifunga bao la kwanza kwa kichwa safi baada ya mpira wa adhabu uliopigwa vizuri na Hannibal Mejbri. Bao hilo liliwapa Tunisia imani mpya na kuongeza presha kwa Nigeria.

Dakika 10 baadaye, Tunisia walipata bahati nyingine baada ya VAR kuamua kuwa Bright Osayi-Samuel alichezea mpira kwa mkono ndani ya eneo la hatari. Ali Abdi alisimama kwenye mkwaju wa penalti na kuupiga mpira kwa nguvu hadi juu ya nyavu, na kuifanya mechi kuwa ya kusisimua zaidi huku Nigeria wakianza kuhofia kupoteza ushindi.

Katika muda wa nyongeza, Tunisia walikaribia kusawazisha baada ya nahodha Ferjani Sassi kupiga kichwa kilichopita karibu sana na lango, lakini bahati haikuwa upande wao. Nigeria walivumilia presha hiyo na hatimaye wakahakikisha wanapata ushindi wao wa pili mfululizo.

Teamwork πŸ‡³πŸ‡¬ 1

Matokeo hayo yameifanya Nigeria kufikisha pointi sita na kuongoza Kundi C, huku wakijiweka katika nafasi nzuri kuelekea mchezo wao wa mwisho dhidi ya Uganda utakaochezwa Fez Jumanne ijayo. Tunisia, waliobaki na pointi tatu, watalazimika kusafiri kwenda Rabat kwa ajili ya mechi muhimu dhidi ya Tanzania, mchezo ambao utakuwa wa kuamua hatma yao katika mashindano hayo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Ademola Lookman aliyeteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi alisema β€œTumefurahia sana kiwango chetu leo. Tumepata pointi tatu, hilo ndilo jambo muhimu zaidi. Tunachukua mazuri na kusonga mbele. Victor ni mshambuliaji mzuri sana na tuna uhusiano mzuri uwanjani. Popote ninapoweza kusaidia timu nafanya hivyo. Kwa sasa nacheza karibu zaidi na lango, hali inayoniwezesha kuwaumiza wapinzani zaidi, na ninafurahia hilo.”

Naye Kocha wa Nigeria, Eric Chelle, alisema β€œNinafuraha na kiwango cha nguvu tulichoonyesha kwa dakika 75. Tulirejesha mpira vizuri juu na chini ya uwanja. Tulishambulia kwa kasi na pia kudhibiti mpira kwa muda mrefu. Tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga. Mpaka dakika ya 75, tulistahili kushinda. Baada ya hapo, Tunisia walionyesha tabia yao ya kupambana. Hata hivyo, tulikuwa timu bora kwa ujumla, ingawa ningependa kumaliza mechi bila kuteseka sana.”

Kwa upande wa Tunisia, kocha Sami Trabelsi alisema maumivu ya kipigo hicho bado yapo, lakini anaona mwanga wa matumaini β€œTuna maumivu makubwa baada ya mechi hii. Dakika za mwisho tulicheza kwa kiwango cha juu, tulitengeneza nafasi nyingi na kufunga mabao mawili. Matokeo yangeweza kuwa tofauti. Lakini upande mzuri ni kwamba tumethibitisha tunaweza kushindana na timu yoyote tukicheza kwa mtindo wetu. Mechi ijayo itakuwa ya maamuzi makubwa.”

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks