Ripoti ya Pedro Kuondoka na Watatu Yanga Sc

Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves ameanza kwa kasi kazi yake ndani ya kikosi hicho baada ya kukipima kikosi hicho kwa macho na takwimu katika mechi sita alizokisimamia, kisha kuwasilisha ripoti nzito kwa uongozi wa klabu hiyo akitaka kuongezewa nguvu kwa kusajili wachezaji watatu wapya ili kukamilisha mipango yake ya kiufundi.
Pedro, raia wa Ureno, ameiongoza Yanga katika mechi nne za Ligi Kuu Bara pamoja na mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, mechi zilizompa picha halisi ya ubora wa kikosi alichokikuta, maeneo yenye changamoto na namna anavyotaka kukibadilisha ili kiwe tishio zaidi ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, kocha huyo amesisitiza anahitaji “mashine” tatu mpya zitakazoongeza nguvu kwenye maeneo muhimu ya uwanja, huku akieleza wazi kuwa maboresho hayo ni muhimu kabla ya michuano kurejea tena baada ya mapumziko.

Eneo la kwanza alilolenga Pedro ni kiungo mkabaji. Ingawa amempongeza Duke Abuya kwa kazi kubwa anayoifanya katika nafasi hiyo, kocha huyo anaamini Yanga inahitaji kiungo mkabaji mwenye ubora wa juu zaidi, mwenye uwezo wa kulinda safu ya ulinzi, kusoma mchezo na kuanzisha mashambulizi kwa haraka.
Pedro amependekeza endapo atapata kiungo mkabaji huyo mpya, basi Abuya atahamishwa kucheza mbele kidogo, akipewa majukumu ya kiungo wa kati anayeshambulia na kusaidia kuzuia. Mpango huo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, utaifanya Yanga kuwa na nguvu maradufu katikati ya uwanja kutokana na uwezo wa Abuya katika kupandisha mashambulizi sambamba na nidhamu ya kiungo mkabaji mpya atakayesajiliwa.
Mbali na kiungo mkabaji, Pedro pia ametaja wazi anahitaji kiungo mshambuliaji halisi, yaani namba 10. Kocha huyo bado haridhishwi na kiwango cha wachezaji waliopo katika eneo hilo, akiamini Yanga inahitaji mchezaji mwenye maamuzi ya haraka, pasi za mwisho zenye macho na uwezo wa kufunga mabao akiwa nje ya boksi.
Katika ripoti hiyo, Pedro ameweka msimamo kuwa hataki kumtumia Pacome Zouzoua kama namba 10, licha ya uwezo mkubwa alionao. Badala yake, kocha huyo anapanga kumtumia kiungo huyo raia wa Ivory Coast kama kiungo wa pembeni, akitokea upande wa kushoto na kucheza katika eneo la nusu (half space).
Kwa mujibu wa Pedro, nafasi hiyo itamfanya Zouzoua kuwa hatari zaidi mbele ya lango la mpinzani kutokana na uwezo wake wa kupiga chenga, kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao. Mpango huo unaonekana tayari kuzaa matunda kwani Zouzoua ameshafunga mabao mawili na kutoa asisti mbili tangu aanze kutumika kwa majukumu mapya.
Hata hivyo, mpango wa kusaka namba 10 mpya unawaweka katika mazingira magumu Mamadou Doumbia na Lassine Kouma, ambao wamekuwa wakipewa nafasi kwa nyakati tofauti kucheza nafasi hiyo. Pia Ecua Celestine, ambaye kwa asili ni namba 10, kwa sasa anachezeshwa pembeni kama winga, jambo linaloashiria mabadiliko makubwa ya kikosi chini ya Pedro.
Eneo la tatu alilolenga kocha huyo Mreno ni winga. Pedro anataka kusajiliwa winga mmoja mwenye ubora wa juu, kasi, uwezo wa kupiga chenga na kuzalisha mashambulizi mengi kutoka pembeni. Anaamini Yanga bado inahitaji mchezaji wa aina hiyo ili kuongeza tishio katika safu ya ushambuliaji hasa dhidi ya timu zinazocheza kwa kujilinda.
Katika hatua ya utekelezaji wa mapendekezo hayo, tayari majina kadhaa ya wachezaji yameanza kuhusishwa na Yanga. Straika Depu na Gelson Dala, wote raia wa Angola, wanatajwa kuwa kwenye rada ya mabosi wa Jangwani, huku Allan Okello kutoka Uganda na Luis Miquissone wa Msumbiji nao wakitajwa kama sehemu ya mipango ya usajili.
Kwa ujumla, ripoti ya kwanza ya Pedro Goncalves imeonyesha wazi falsafa yake ya soka na namna anavyotaka kuijenga Yanga kuwa timu imara, yenye kasi, ubunifu na uwezo wa kushindana katika viwango vya juu barani Afrika. Sasa macho na masikio yote yapo kwa mabosi wa klabu hiyo kuona kama watatimiza ombi la kocha wao na kumletea “mashine” tatu alizozitaka ili amalize kazi.
