Tanzania Yatolewa Kibabe Afcon 2025

www.sportsleo.co.tz

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeaga mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa Jumapili usiku kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, Rabat.

Licha ya kupoteza, Taifa Stars ilionesha upinzani mkubwa na kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu dhidi ya Atlas Lions, mbele ya maelfu ya mashabiki wa Morocco waliokuwa wamefurika uwanjani kushangilia timu yao. Mchezo huo ulikuwa na presha kubwa kwa wenyeji waliokuwa wakihitaji ushindi ili kuendelea mbele, huku Tanzania ikisaka kuandika historia na kuthibitisha maendeleo yake kwenye soka la Afrika.

Katika kipindi cha kwanza, Morocco ilishindwa kabisa kupata mpangilio wake wa kawaida kutokana na presha kubwa kutoka kwa wachezaji wa Tanzania. Taifa Stars ilimiliki sehemu kubwa ya mchezo, ikicheza kwa kujiamini na kuzuia njia zote za mashambulizi ya wenyeji. Ulinzi wa Tanzania uliongozwa vyema na mabeki wake waliokuwa makini na waliocheza kwa kujituma, hali iliyowafanya nyota wa Morocco kushindwa kupenya kirahisi.

Morocco ilidhani imepata bao la kuongoza kupitia Ismail Saibari, lakini baada ya mwamuzi kushauriana na mfumo wa VAR, bao hilo lilikataliwa kwa sababu ya kuotea. Tukio hilo liliongeza morali kwa wachezaji wa Tanzania ambao waliendelea kucheza kwa nidhamu na mshikamano mkubwa hadi mapumziko, huku matokeo yakiwa sare tasa.

35d5dde0 e996 11f0 8c13 1355ac9f9bd1.jpg

Kipindi cha pili kilianza kwa Morocco kuongeza kasi ya mashambulizi, lakini bado Taifa Stars iliendelea kujilinda kwa umakini mkubwa. Dakika ya 55, Tanzania ilipata nafasi adhimu ya kufunga bao baada ya kiungo mahiri Faisal Salum kupokea pasi nzuri ndani ya boksi la Morocco, lakini alishindwa kuutumia vizuri mpira huo baada ya kupiga shuti lililopita pembeni mwa lango.

Dakika nane baadaye, Morocco ilipata bao la ushindi kupitia nyota wake Brahim Diaz, aliyefanya kazi ya ziada binafsi kwa kuingia ndani ya boksi kwa pembe finyu na kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Tanzania, Hussein Masalanga. Bao hilo liliamsha shangwe kubwa kwa mashabiki wa wenyeji na kuwapa Morocco uongozi uliodumu hadi mwisho wa mchezo.

Baada ya bao hilo, Morocco iliendelea kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga, ikiongozwa na nahodha wao Achraf Hakimi aliyerejea uwanjani baada ya kuwa nje kwa majeraha. Hata hivyo, Taifa Stars ilisimama imara na kuendelea kupambana, ikionesha moyo wa kupigania bendera ya taifa na ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa ushindi huo, Morocco imeungana na Senegal na Mali kufuzu hatua ya robo fainali, huku ikisubiri kukamilika kwa michezo mingine ya hatua ya 16 bora. Licha ya kuondolewa, Tanzania imeondoka kifua mbele baada ya kuonyesha kiwango bora dhidi ya moja ya timu kubwa barani Afrika.

Mmoja wa mashabiki wa Morocco, Hussein Ahmad, aliisifu Tanzania kwa kiwango ilichoonyesha. “Timu ya Tanzania imecheza vizuri sana na ilistahili kufika hatua ya mtoano. Wamebeba vyema bendera ya Afrika Mashariki,” alisema Hussein akizungumza na Cecafaonline.

Kocha mkuu wa Taifa Stars, Miguel Ángel Gamondi, alisema anajivunia wachezaji wake kwa kujituma na kupambana hadi mwisho. “Wachezaji wangu walionesha dhamira na nidhamu kubwa uwanjani. Tumeonyesha kuwa pengo kati yetu na Morocco si kubwa kama watu wengi wanavyodhani,” alisema Gamondi.

Gamondi aliongeza kuwa mchezo huo ni somo muhimu kwa Tanzania kuelekea mashindano yajayo, akisisitiza kuwa Taifa Stars ina msingi mzuri wa kujenga timu imara zaidi kwa siku zijazo.

Kwa ujumla, safari ya Tanzania AFCON 2025 imeacha taswira chanya kwa mashabiki wa soka nchini, ikionesha kuwa Taifa Stars ina uwezo wa kushindana na vigogo wa soka la Afrika, endapo itaendelea kupewa maandalizi na sapoti stahiki.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks