Pamba Jiji Fc Yaikazia Singida BS

Katika mchezo uliogubikwa na ushindani mkali na kasi ya aina yake, Pamba Jiji FC imeendelea kuonesha kuwa si timu ya kubezwa msimu huu baada ya kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Singida Black Stars katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, kwenye muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Ingawa walionekana kupwaya dakika za awali, morali ya vijana wa “Tp Lindanda” iliwafanya wapiganie kila mpira, na hatimaye kuandika matokeo muhimu mbele ya mashabiki wao waliofurika uwanjani.
Mchezo huo uliokuwa na dakika 90 za msisimko, uliweka hadharani ubora wa kiufundi wa timu zote mbili,moja ikiwania kubaki kileleni, na nyingine ikiwa na kiu ya kuonesha huwezi kuitabiria matokeo kirahisi.
Chama awasha moto dakika ya 33
Kocha wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi, alianza mchezo kwa kuonyesha mpira wa kushambulia kwa pasi fupifupi na kasi katika wingi wa mawinga.
Mkufunzi huyo ambaye amepewa jukumu la kuwarejesha Black Stars kwenye ubora wao, alionekana kutawala mchezo kwa dakika nyingi za mwanzo.
Mkali wao kwenye kiungo, Clatous Chama, ambaye ndiye alama ya ubunifu katika timu hiyo, alivunja ukuta wa Pamba Jiji dakika ya 33 kwa shuti adhimu lililopigwa kwa ustadi wa hali ya juu na kumshinda kipa wa Pamba, na kuwapa wageni bao la kuongoza. Bao hilo liliibua shangwe kubwa kwa mashabiki wachache wa Singida waliofika uwanjani, huku presha ikiongezeka kwa wenyeji.
Goli hilo lilionekana kuwa kama alama ya kuanza kuporomoka kwa Pamba Jiji, lakini wakati wengi wakidhani hivyo, kocha wao aliwamotisha vijana wake na kuhimiza mpira wa kushambulia zaidi kupitia pande zote mbili.
Kelvin Nashon apiga la kisasi dakika ya 51
Kipindi cha pili kilipoanza, Pamba Jiji walirudi uwanjani wakiwa na sura tofauti kabisa. Waliongeza mashambulizi, kiwango cha mbinu kikabadilika, na mashabiki wakaanza kujawa na matumaini mapya.
Dakika ya 51, mchezaji wao Kelvin Nashon akiwa ni usajili wao kwa mkopo kutoka Singida Black Stars aliandika historia Baada ya kupokea mpira safi ndani ya eneo la hatari, Nashon alisalimuisha kipa wa zamani wake kwa shuti lililoenda moja kwa moja wavuni na kuwafanya mashabiki wa Kirumba kuripuka kwa furaha.
Bao hilo lilikuwa na uzito wa aina yake: silaha ya zamani kuisumbua timu yake ya asili ndiyo stori iliyovutia wengi, na kufanya mchezo kuwa na ladha ya kipekee.
Nashon si tu alisawazisha, bali alionesha ukomavu na ubora uliomshawishi kocha wake kumtumia kama chaguo la kwanza katika kikosi.
Simba wawili ambao hawatakubali kuanguka kirahisi
Baada ya kusawazisha, mchezo uliendelea kwa kasi kubwa. Black Stars walijaribu kurudi mchezoni kwa nguvu, huku Chama akiendelea kuwa injini ya timu. Hata hivyo, ngome ya Pamba ikiongozwa na mabeki wao imara ilizuia kila jaribio kwa nidhamu ya hali ya juu.
Kocha Gamondi alionekana kukata tamaa taratibu baada ya washambuliaji wake kushindwa kuvunja ukuta wa Pamba Jiji, na mwisho wa dakika 90, timu hiyo ililazimika kuondoka Kirumba na alama moja tu si matokeo aliyotarajia.
Nafasi kwenye msimamo wa ligi
Kutokana na sare hiyo sasa Singida Black Stars ipo nafasi ya 6 ya ligi kuu ikiwa na alama 7 baada ya kucheza Mechi 3 huku Pamba Jiji FC ipo katika nafasi ya 2 ikiwa na alama 9 baada ya kucheza mechi 6 za ligi kuu ya Nbc nchini.
Takwimu hizi zinaonesha kikosi cha Pamba Jiji kikiwa kimecheza michezo zaidi, lakini kikionyesha uthabiti wa kupigania nafasi za juu msimu huu.
Kelvin Nashon, Mchezaji Bora wa Mchezo
Hakuwa tu mkombozi wa Pamba Jiji, bali pia alichukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Mchezo kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya dakika zote alizocheza. Alikuwa tishio kwa mabeki wa Singida Black Stars kila alipogusa mpira.
Kwa ujumla, sare hii imeweka msisimko mpya kwenye ligi, na kama kasi hii itaendelea, Pamba Jiji wanaweza kuwa moja ya timu zitakazotia chachu na presha kwenye mbio za ubingwa. Wakati huo huo, Black Stars watahitaji kurekebisha makosa ili kurejea kwenye matarajio yao ya kusaka nafasi ya juu.


