Hali ni tete katika kambi ya timu ya Tabora United kufuatia mastaa wa timu hiyo kutishia kugomea mchezo wa mwisho wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union mpaka pale madai yao ya mishahara yatakapolipwa.
Kikosi cha Tabora United kilipaswa kusafiri juni 20 2025 asubuhi kuelekea Tanga kwa ajili ya mchezo wa mwisho dhidi ya Coastal Union ila bado Kipo Dar Es Salaam na wachezaji wamegoma hadi walipwe kiasi cha mshahara kilichobaki.
Wachezaji wa Tabora Utd mwanzo baada ya kugoma walilipwa mshahara nusu wa mwezi mmoja pamoja na kuahidiwa wakifika Dar Es Salaam kwenye mchezo dhidi ya Azam FC kabla ya kusafiri kwenda Tanga kucheza dhidi ya Coastal Union watakuwa wamelipwa mshahara nusu uliobaki na mshahara wa mwezi mwingine ambao ulikuwa haujalipwa kabisa.
Licha ya juhudi za Viongozi wa Tabora Utd kupiga simu kwa kila mchezaji kuwaomba waende Tanga kumalizia ligi kuu ya NBC na watalipa pesa za mshahara zilizobaki wiki ijayo bado hali imekua ngumu baada ya mastaa kukaza.
Tayari mshambuliaji Heritier Makambo ameshajiondoa kabisa klabuni hapo baada ya madai mengi ya mshahara na pesa baadhi za usajili ambazo hajalipwa hivyo hatakuwepo mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Coastal Union na ameshamalizana na timu hiyo ambapo pia mkataba wake umefikia kikomo.