Okello Aizamisha Uganda,Aipa Alama Moja Tanzania

Mastaa wa kimataifa wajiunga na Stars kuelekea Morocco kwa maandalizi makubwa

Kukosa kwa penati ya dakika za majeruhi kulikofanywa na Allan Okello kumeigharimu vibaya Uganda baada ya kutoka sare ya 1–1 dhidi ya Tanzania katika dabi kali ya Afrika Mashariki, mchezo wa Kundi C wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayodhaminiwa na TotalEnergies, uliochezwa usiku wa Jumamosi katika Uwanja wa Stade El Barid, Rabat, Morocco.

Uganda walikuwa na nafasi ya dhahabu ya kuondoka na pointi zote tatu baada ya mshambuliaji wa akiba Karl Ikpeazu kusawazisha bao na kufuta uongozi wa Tanzania uliopatikana kupitia Simon Msuva. Hata hivyo, ndoto ya ushindi wa kusisimua ilizimwa katika sekunde za mwisho baada ya Okello kupiga penati iliyokwenda juu ya lango, na kuwaacha Cranes wakijilaumu.

Ushindi ungeongeza kwa kiasi kikubwa matumaini ya Uganda ya kufuzu hatua ya mtoano, lakini sare hiyo sasa inaacha Tanzania na Uganda katika mazingira magumu, wakilazimika kushinda michezo yao ya mwisho ya kundi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.

b25l1ss3172

Mchezo huo uliishi kulingana na matarajio ya dabi ya kikanda, ukiwa na ushindani mkali, kasi kubwa na presha ya hali ya juu. Kipindi cha kwanza kilishuhudia Uganda wakitawala sehemu kubwa ya umiliki wa mpira, huku Rodgers Mato akiwa karibu kuifungia Uganda bao la mapema baada ya kichwa chake kikali kutoka kwa krosi ya Azizi Kayondo kugonga mwamba wa lango.

Allan Okello pia aliipima safu ya ulinzi ya Tanzania mara mbili, akimlazimisha kipa Foba Zuberi kufanya kazi ya ziada kuokoa mashuti ya karibu. Licha ya presha hiyo, Tanzania waliinuka kwa nidhamu ya hali ya juu, wakiongozwa na uzoefu wa mshambuliaji Simon Msuva aliyekua mwiba kwa mabeki wa Uganda akifanya mashambulizi ya kasi mara kwa mara.

Baada ya mapumziko, kasi ya mchezo iliendelea kuwa ya juu, huku Tanzania wakionekana kubadilika kiufundi na kuanza kushambulia kwa mpangilio zaidi. Mabadiliko hayo yalizaa matunda dakika ya 58, pale beki wa Uganda Alhassan Baba alipochezea mpira kwa mkono ndani ya eneo la hatari akijaribu kuzuia shuti la Alphonce Msanga.

Mwamuzi hakusita kuashiria penati, na Simon Msuva, winga mwenye uzoefu mkubwa wa michuano mikubwa, alichukua jukumu hilo kwa kujiamini na kuupiga mpira kwa umakini, akimzidi maarifa Onyango na kuipatia Tanzania bao la kuongoza.

Total Energies AFCON 2025 70 Uganda 🇺🇬 0️⃣ 1️⃣ 🇹🇿@TaifaStars Msuva ⚽️ @taifastars @nsc b

Bao hilo liliwapa Tanzania nguvu na kujiamini, lakini Uganda hawakukata tamaa. Wakiongeza presha na kasi ya mashambulizi, walipata bao la kusawazisha dakika10 kabla ya mchezo kuisha kupitia Ikpeazu, aliyeruka na kuunganisha krosi safi ya Dennis Omedi kwa kichwa, na kuamsha shangwe miongoni mwa mashabiki wa Cranes.

Dakika zilizofuata zilikuwa za kupokezana mashambulizi, kila timu ikitafuta bao la ushindi. Uganda walionekana kuwa karibu zaidi kufunga bao la pili, hasa walipopata penati katika dakika za mwisho za nyongeza. Hata hivyo, Okello, aliyekuwa shujaa mtarajiwa, alipoteza mwelekeo na kuupiga mpira juu ya lango, na kusababisha majonzi makubwa kwa benchi la Uganda.

Bado kulikuwa na nafasi kwa Tanzania kupata bao la pili, baada ya Onyango kuacha mpira uliovuka hatari ndani ya eneo, lakini mshambuliaji wa Tanzania, Charles M’Mbowa, alipiga shuti lililotoka nje kidogo, na kuinusuru Uganda dhidi ya adhabu ya dakika za mwisho.

Mchezaji Bora wa Mechi (MOM): Simon Msuva – Tanzania
Baada ya mchezo kumalizika Msuva alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo na maofisa wa Caf ambapo alisema kuwa “Nashukuru sana. Nimefurahi kupata tuzo hii, lakini siwezi kuchukua sifa zote. Ni kwa ajili ya wachezaji wenzangu na mashabiki waliotusapoti. Tulijua Uganda ni majirani zetu hivyo mchezo ungekuwa mgumu, lakini kwa pamoja tulifanya kazi na kupata matokeo,” alisema Msuva.

Tanzanias Simon Msuva earns the TotalEnergies Man of the Match award with a standout performanc

Naye kocha wa Tanzania Miguel Gamondi baada ya dakika 90 za mchezo huo alisema kuwa “Kwanza, tunajisikia kukata tamaa kidogo kwa sababu hatukushinda, lakini naamini tulicheza mchezo mzuri sana wenye kasi kubwa. Katika kushambulia tulipoteza mipira baadhi. Uganda walitengeneza nafasi nzuri, lakini nadhani tulibadilika vizuri kipindi cha pili. Tulitengeneza nafasi, tulitawala na tulikuwa hatari, ila tulifanya kosa moja lililosababisha bao. Tunaomba radhi kwa Watanzania kwa kutoshinda, lakini tunaendelea kufanya kazi kwa bidii kwenye mashindano haya magumu.”

Kocha wa timu ya Taifa ya Uganda Paul Putt naye hakua nyuma akisema kuwa walistahili ushindi katika mchezo huo “Nafikiri hatukustahili sare. Tulikuwa na nafasi nyingi zaidi na umiliki mkubwa wa mpira. Pia tumekosa penati, jambo ambalo linaumiza sana, lakini hiyo ni sehemu ya soka. Tuna timu changa sana, na jukumu langu pia ni kujenga timu kuelekea 2027 kwa kuwa sisi ni wenyeji. Nimewaambia wachezaji waendelee kuamini, kwa sababu bado kuna mchezo mmoja. Tumeumia, lakini tunahitaji kubadilisha mawazo na kujiandaa dhidi ya Nigeria, ambao tunajua hawatakuwa rahisi.”

Baada ya sare hiyo, Tanzania sasa wanajiandaa kwa mtihani mgumu dhidi ya Tunisia katika Uwanja wa Olympic siku ya Jumanne, huku Uganda wakisafiri kwenda Fez kukutana na Nigeria, mchezo unaotajwa kuwa wa kuamua hatma ya kundi hilo.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks