Aziz KI Afunguka Ndoa Yake na Hamisa, Amwagia Sifa Fei Toto

Kiungo mahiri wa Wydad Athletic Club ya Morocco, Stephane Aziz KI, amefunguka kwa kina kuhusu maisha yake ya ndoa na mke wake, mwanamitindo maarufu wa Tanzania, Hamisa Mobetto, akisema kuwa watu wengi hawamfahamu vyema kiundani, kwani ni mtu tofauti kabisa na taswira inayowaonekana hadharani.
Aziz KI amesema kuna tofauti kubwa kati ya Hamisa anayemuona umma na yule wa ndani ya nyumba, akieleza kuwa ni mwanamke mkarimu, mwenye mapenzi ya dhati, anayejali familia na mwenye hofu ya Mungu, sifa ambazo ndizo zilizomfanya achukue uamuzi wa kumuoa bila kusita.

“Nina uhakika asilimia 90 watu hawamjui vizuri mke wangu. Hawajui namna alivyo mkarimu na mtu anayenisapoti kwa kiwango kikubwa. Hata mimi wakati naanza naye nilishtuka sana, kwa sababu sikuwa namjua Hamisa wa ndani, nilikuwa namjua yule wa nje tu,” amesema Aziz KI.
Ameongeza kuwa kadri walivyozidi kuendelea na mahusiano, ndivyo alivyogundua utu na upendo wa kweli alionao mke wake, jambo lililompa uhakika wa kufanya uamuzi sahihi wa kuingia kwenye ndoa.
“Ni mtu tofauti na huyu mnayemuona nje. Akiwa nyumbani ni mama wa familia, anajali sana, ni mtu mzuri na mcha Mungu. Kwangu mimi ilikuwa ni uamuzi sahihi kumuoa. Ilikuwa rahisi kwa sababu alinionyesha tabia zake halisi mapema na nikajiridhisha kuwa ni mtu sahihi. Namshukuru Mungu sana na ninampenda kwa dhati,” amesema.
Akizungumzia safari ya mipango ya ndoa yao, nyota huyo wa Wydad amesema haikuwa ngumu kama watu wengi wanavyodhani, kwani Hamisa alimfanya kila kitu kiwe rahisi kutokana na namna alivyokuwa anamwelewa na kumsapoti katika maisha yake ya soka na nje ya uwanja.
“Ilikuwa rahisi kwa sababu alifanya kila kitu kuwa chepesi kwangu. Ni mtu ambaye alibadilisha maisha yangu, kuna namna yamekuwa ya furaha zaidi tangu tumekuwa pamoja. Naweza kusema kabla ya kuwa naye maisha yalikuwa ya kawaida, lakini sasa kuna amani, furaha na utulivu zaidi,” amesema Aziz KI.
Mbali na kuzungumzia maisha yake binafsi, Aziz KI pia alitumia nafasi hiyo kumsifia kiungo wa Azam FC na Taifa Stars, Feisal Salum ‘Fei Toto’, akisema ni mmoja wa wachezaji waliopata misingi mizuri ya mpira wa miguu tangu wakiwa chini, hali inayojidhihirisha katika aina ya uchezaji wake.

Aziz KI amesema anapomwangalia Fei Toto, huona picha halisi ya kile kinachoweza kupatikana iwapo vipaji vya Tanzania vitawekewa mazingira sahihi ya kukuza uwezo wao tangu wakiwa wadogo.
“Nikimuangalia mchezaji kama Feisal Salum, huwa naamini kabisa Tanzania kuna wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa, tatizo ni mazingira. Kuna vipaji vingi sana, lakini havijatengenezewa mazingira mazuri ya kuvikuza,” amesema.
Amefafanua kuwa tofauti ya Fei Toto na wengine ni misingi aliyopata tangu akiwa mdogo, jambo linalompa uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi sahihi akiwa na mpira, kusogea kwa akili na kuisoma michezo kwa wepesi.
“Ukimwangalia Fei Toto unaona wazi kuwa mbali na kipaji alichonacho, aliandaliwa vizuri kutoka chini. Ana malezi ya soka ambayo hata mimi niliyapata nikiwa mdogo. Unamuona namna anavyoweza kusogea na mpira, anavyofanya maamuzi kwa haraka na kwa usahihi. Hayo yote ni matokeo ya maandalizi ya muda mrefu,” amesema.
Nyota huyo wa Wydad amesisitiza kuwa ili Tanzania ipate wachezaji wengi wa kiwango cha Fei Toto, ni lazima uwekezaji mkubwa ufanyike kwenye soka la vijana, kuanzia umri mdogo, hususan kuanzia miaka 15 na chini.
“Ukianza kuwajenga watoto kuanzia umri mdogo, miaka 15 au chini, utapata wachezaji wazuri sana ambao baadaye watakuja kuichezea Taifa Stars. Lakini lazima wapewe mazoezi sahihi na walimu bora wa mpira,” amesisitiza.
Aziz KI pia aligusia umuhimu wa elimu kwa wachezaji chipukizi, akisema soka peke yake halitoshi, bali mtoto anatakiwa kujengwa kiakili na kielimu ili awe na maisha bora hata baada ya kumaliza soka.
“Mtoto lazima apewe mazoezi mazuri yanayostahili, lakini pia apate elimu ya shule. Elimu ni muhimu sana kwa sababu kuna maisha baada ya soka. Mchezaji anatakiwa kujengwa kiakili, ajue kuwajibika na kuelewa maisha kwa upana zaidi,” amesema.
Kwa mtazamo wake, mchanganyiko wa elimu, malezi bora ya soka na mazingira mazuri ya kukuza vipaji ndio msingi wa kuzalisha wachezaji wenye uwezo wa kucheza ndani na nje ya nchi, huku Taifa Stars ikinufaika kwa muda mrefu.
Kauli za Aziz KI zinaongeza uzito katika mjadala wa maendeleo ya soka la Tanzania, huku zikionesha pia upande wake wa kibinadamu nje ya uwanja, kama mchezaji anayethamini familia, maadili na maendeleo ya vijana kupitia michezo.

