TRA United Wamuwinda Nkane kwa Mkopo

Dont forget why you started

Uongozi wa klabu ya TRA United, maarufu kama Mabosi wa Kodi na waliokuwa wakijulikana zamani kama Tabora United, umeanza harakati za kuangalia uwezekano wa kumnasa kwa mkopo nyota wa Young Africans (Yanga), Denis Nkane, katika dirisha dogo la usajili linaloendelea, baada ya mchezaji huyo kushindwa kupata nafasi ya mara kwa mara ndani ya kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya TRA United zinaeleza kuwa hatua ya kuanza mazungumzo ya awali kuhusu Nkane imechochewa zaidi na sintofahamu ya hatma ya aliyekuwa mshambuliaji wao tegemeo, Emmanuel Mwanengo, ambaye inadaiwa tayari ameshasaini mkataba wa kujiunga na Yanga na muda wowote kuanzia sasa anatarajiwa kutambulishwa rasmi kama mchezaji mpya wa Wananchi.

Kupotea kwa Mwanengo, ambaye alikuwa mhimili mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya TRA United, kumeifanya klabu hiyo kuanza upya mchakato wa kusaka mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja, jambo linalomfanya Nkane kuonekana kama chaguo sahihi kutokana na uzoefu wake na uwezo wake wa kubadilika kulingana na mahitaji ya timu.

Dont forget why you started 1

Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, mmoja wa viongozi wa juu wa TRA United alithibitisha kuwepo kwa mazungumzo hayo, akisema kuwa ingawa bado hayajafikia hatua ya mwisho, nia ya klabu ni dhahiri na mchezaji huyo yupo katika orodha ya vipaumbele vya usajili.

“Ni kweli kabisa kuna mazungumzo ya awali kuhusu Denis Nkane. Ni mchezaji tunayemfahamu vizuri na tunaamini anaweza kuongeza kitu kikubwa ndani ya kikosi chetu kutokana na uzoefu wake wa kucheza katika timu kubwa kama Yanga,” amesema kiongozi huyo.

Aliongeza kuwa, hata hivyo, uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya usajili wa mchezaji huyo utategemea mapendekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha mkuu wa timu hiyo, Etienne Ndayiragije raia wa Burundi, ambaye amepewa mamlaka makubwa katika masuala ya usajili.

“Kama uongozi, jukumu letu ni kufungua milango na kuangalia uwezekano, lakini maamuzi ya mwisho yapo mikononi mwa benchi la ufundi. Kocha ndiye anayejua aina ya mchezaji anayehitaji kulingana na falsafa yake ya soka,” alisisitiza.

TRA United ilimnasa Ndayiragije hivi karibuni akitokea Police FC ya Kenya, klabu aliyoiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya msimu wa 2024/2025, mafanikio yaliyompa heshima kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kiongozi huyo wa TRA United alisema kati ya makubaliano muhimu waliyofikia na kocha huyo ni kumpa uhuru mpana wa kufanya usajili wa wachezaji anaowaona wanafaa kuijenga timu kwa mtazamo wake.

“Wakati tunafanya mazungumzo ya mkataba wake, alituweka wazi vipaumbele vyake, nasi tukamuwekea wazi matarajio yetu. Moja ya mambo aliyosisitiza sana ni apewe uhuru wa kufanya usajili, hasa katika dirisha dogo, ili aweze kurekebisha kikosi kulingana na mahitaji ya ushindani wa ligi,” amesema.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, uongozi wa klabu haukuona tatizo katika ombi hilo kwa kuwa una imani kubwa na uwezo wa Ndayiragije kutokana na rekodi yake ya kazi na falsafa yake ya kuendeleza wachezaji.

Kwa upande wa Yanga, Nkane amekuwa akipata ugumu wa kupata nafasi ya mara kwa mara kutokana na ushindani mkubwa uliopo katika kikosi hicho, hususan katika maeneo anayoweza kucheza. Mchezaji huyo ana uwezo wa kucheza kama beki wa kulia, winga wa pembeni pamoja na kiungo mshambuliaji, hali inayomfanya awe na thamani kubwa, lakini pia inamkutanisha na wachezaji wengi wenye ubora wa juu katika nafasi hizo.

Nkane alijiunga na Yanga Januari Mosi, 2022 akitokea Biashara United, akiwa na matarajio makubwa ya kung’ara ndani ya klabu hiyo kongwe. Tangu wakati huo amekuwa sehemu ya mafanikio ya Wananchi, ingawa msimu wa hivi karibuni amejikuta akitumika zaidi kama mchezaji wa akiba.

Iwapo dili la mkopo litakamilika, Nkane anaweza kupata nafasi ya kucheza kwa dakika nyingi zaidi ndani ya TRA United, huku klabu hiyo ikinufaika na uzoefu na uwezo wake wa kucheza nafasi tofauti, jambo linaloweza kuipa nguvu mpya katika mbio za ligi msimu huu. Macho na masikio sasa yanaelekezwa katika uamuzi wa mwisho wa benchi la ufundi na msimamo wa Yanga juu ya kumruhusu nyota huyo kuondoka kwa mkopo.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks