Ibenge Afunguka Kukutana na Simba Sc

610669714 18547665247052678 133177792393917480 n

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema mechi ya kesho dhidi ya Simba SC haiwezi kufananishwa kwa namna yoyote na ile ya mwisho walipokutana katika Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini amesisitiza kuwa katika suala la matokeo, malengo ya Azam yamebaki kuwa yaleyale kushinda na kufuzu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa nusu fainali wa michuano hiyo, Ibenge alisema licha ya Azam kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba katika mchezo wa ligi uliochezwa Desemba 7, 2025, historia hiyo haina nafasi kubwa katika maandalizi ya mchezo wa kesho unaotarajiwa kuchezwa Alhamisi usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, kuanzia saa 2:15 usiku.

587744186 18543559357052678 6572660750910535961 n

“Tunaiheshimu Simba kama moja ya klabu kubwa nchini Tanzania, sawa kabisa na Yanga. Lakini tumesisitiza kwa wachezaji wangu kuwa wasisahau mechi iliyopita kwa matokeo yake, bali waelewe kuwa kesho ni mchezo mpya kabisa, katika mashindano tofauti, mazingira tofauti na hata wachezaji wanaoweza kuanza hawatakuwa wale wale,” alisema Ibenge.

Kocha huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aliongeza kuwa Kombe la Mapinduzi lina ushindani wake wa kipekee, hasa linapofikia hatua za mtoano, ambapo kosa dogo linaweza kugharimu timu nafasi ya kufuzu. Hivyo, amesema maandalizi ya Azam yamejikita zaidi katika namna ya kuucheza mchezo wa kesho badala ya kuangalia rekodi za nyuma.

“Katika michezo ya nusu fainali hakuna nafasi ya kufanya makosa mengi. Tunajua Simba wana uzoefu mkubwa katika mechi za aina hii, wana wachezaji wenye ubora na wanaweza kubadilisha matokeo muda wowote. Ndiyo maana tumejiandaa kisaikolojia na kiufundi kuhakikisha tunacheza kwa nidhamu ya juu,” aliongeza.

Ibenge pia alieleza kuwa licha ya kutofautiana kwa aina ya mchezo, Azam inaingia uwanjani ikiwa na lengo moja kuu kufuzu fainali na kupigania taji la Kombe la Mapinduzi. Alisisitiza kuwa ushindi dhidi ya Simba kwenye ligi hauwapi Azam faida yoyote ya ziada katika mechi ya kesho, zaidi ya kuwapa ujasiri wa kupambana.

“Matokeo ya ligi hayabadilishi chochote kesho. Simba ni Simba, na Azam ni Azam. Hii ni nusu fainali, mshindi anaenda fainali, aliyepoteza anaondoka. Hilo ndilo jambo muhimu zaidi,” alisema kwa msisitizo.

Kocha huyo pia alizungumzia suala la mzunguko wa wachezaji (rotation), akisema ni jambo la kawaida katika mashindano ya aina hii, hasa kutokana na ratiba ya mechi zinazokaribiana. Alibainisha kuwa kikosi chake kina wachezaji wengi wenye uwezo wa kuanza na kumaliza mechi, hivyo hatarajii hilo kuwa changamoto.

Kwa upande mwingine, Ibenge alisema anaifahamu vyema presha inayokuja na mechi dhidi ya Simba, hasa kutokana na historia ya ushindani kati ya timu hizo mbili. Hata hivyo, alisema amewaandaa wachezaji wake kukabiliana na presha hiyo na kuibadilisha kuwa chachu ya kufanya vizuri.

Mechi hiyo ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 inatarajiwa kuwa na mvuto mkubwa, ikizingatiwa ukubwa wa timu zinazokutana na umuhimu wa tiketi ya fainali. Mshindi wa pambano hilo atafuzu kucheza fainali itakayopigwa Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, dhidi ya mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Yanga SC na Singida Black Stars.

Kwa mashabiki wa soka nchini, pambano la Simba na Azam linatajwa kuwa fainali ya mapema, kutokana na ubora wa vikosi vyote viwili na rekodi zao katika mashindano ya ndani. Hata hivyo, kwa mujibu wa Ibenge, mambo yote hayo yataachwa nje ya uwanja, huku kilicho muhimu zaidi kikiwa ni utekelezaji wa mpango wa mchezo ndani ya dakika 90.

“Tunataka kushinda, hilo ndilo lengo letu kuu. Tunaiheshimu Simba, lakini hatuwaogopi. Tutaingia uwanjani kupambana, na timu itakayokuwa bora kesho, itastahili kwenda fainali,” alihitimisha kocha huyo wa Azam FC.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks