Simba Sc Yaanza Safari ya Alama Tatu Mali

Kikosi cha Simba SC kimeanza safari ndefu na yenye presha kuelekea nchini Mali kupitia Ethiopia, tayari kwa mchezo wao wa pili wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji Stade de Malien, mchezo mzito utakaopigwa Jumapili. Huu ni mchezo ambao wamewekewa mzigo mkubwa wa lazima kushinda ili kurejesha matumaini ya mashabiki wao baada ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani.
Msafara wa Simba umeondoka wakiwa na matumaini na wajibu ambapo Matumaini ya kuingia uwanjani na nguvu mpya, na wajibu wa lazima kupata pointi tatu baada ya kutoneshwa nyumbani na Petro Atletico de Luanda kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wiki iliyopita. Kipigo hicho kimewafanya wafuasi wa Msimbazi kukaa kooni, wakisubiri kuona kama safari ya Mali itakuwa zima au vibaya zaidi.
STANDE DE MALIEN WAMEBADILIKA
Kwenye kundi lao, Simba hawaendi kukutana na timu ya kawaida. Stade de Malien wameanza michuano ya msimu huu kwa kiwango kinachotishia wapinzani wote. Hivi karibuni waliilazimisha sare ya 0-0 moja ya timu ngumu zaidi barani Afrika ya Esperance de Tunis. Katika dunia ya CAF, ukimzuia Esperance kupata bao, maana yake una silaha nyingi kupambana nazo.
Kocha wa Simba Goran Pandev anajua wazi mechi hii haitakuwa matembezi ya kunywa maji ya baridi. Ni vita. Ni ‘90 minutes of war.’ Na ni mchezo ambao unaweza kuamua kama Simba watapepea au watabaki kwenye presha mpaka mwisho wa makundi.
MAJERAHA YAWATIKISA—WATATU WABAKIA DAR
Simba wamekuwa na mkosi mdogo wa majeraha kabla ya safari hii muhimu. Wachezaji tatu wamekosekana kwenye msafara kutokana na majeraha yanayowasumbua ambao ni Kipa Mousa Camara Beki Abdulrazack Hamza na Kiungo mshambuliaji Mohamed Bajaber.
Hawa wote wameachwa Dar wakipambana kufikia utimamu wa mwili kabla ya mechi zinazofuata. Kuwaacha nyuma ni pigo, hasa ukizingatia wachezaji kama Camara na Hamza wamekuwa wakitumiwa mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza msimu huu.
Kutokana na pengo hilo, jukumu la kusimama langoni litamuangukia Yakub Seleman pamoja na Hussein Abel, wawili wanaokabiliwa na jukumu zito la kuzuia mashambulizi ya Wamali. Kwa namna Stade de Malien wanavyocheza kwa kasi, makipa hawa watakuwa na siku ngumu kama safu ya ulinzi haitakuwa makini.
SAFU YA ULINZI YOTE SAFARINI
Simba wamesafiri na safu ya ulinzi yenye utulivu na uzoefu. Mabeki waliopo kwenye msafara ambao ni Shomari Kapombe,Anthony Mligo,Rushine De Reuck,Chamue Karaboe,David Kameta ‘Duchu’ na Wilson Nangu.
Hii ndio safu inayotarajiwa kutengeneza ukuta wa chuma mbele ya makipa wao. Wamelazimika kujiandaa na mchezo wenye kasi, presha ya mashabiki wa Mali na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa wenyeji ambao huwa hatari zaidi wakicheza kwenye ardhi yao.
KIUNGO KIMETIMIA
Kiungo ndio moyo wa mchezo wa Simba kila msimu. Katika safari hii, eneo hilo lina wachezaji wengi zaidi ili kutoa chaguo nyingi kwa benchi la ufundi ambapo Yusufu Kagoma, Allasane Kante, Ellie Mpanzu, Naby Camara, Neo Maema, Morice Abraham, Jean Charles Ahoua, Charles Semfuko, Ladack Chasambi, na Joshua Mutale wote wamesafiri.
Wachezaji hawa ndiyo injini ya timu. Wanapaswa kupunguza makosa ya pasi, kuongeza kasi ya mashambulizi na kuisaidia timu kumiliki mpira. Kwa namna Stade de Malien walivyokuwa na nguvu mbele ya Esperance, Simba watapaswa kuwa na utulivu wa hali ya juu na kukaba kwa nidhamu.
PANDEV KUBADILI MFUMO,KUANZA NA WASHAMBULIAJI HALISI
Kwa upande wa washambuliaji, Simba wamechukua silaha zao tatu za kuaminika ambazo ni Jonathan Sowah, Salum Mwalimu, na Steven Mukwala na inaonyesha mwalimu pandev sasa atatumia mshambuliaji halisi tofauti na mchezo uliopita ambapo wote watatu walianzia benchi.
Mukwala, ambaye amekuwa tishio kwenye michuano yote aliyoichezea Simba, anatazamiwa kuongoza safu ya ushambuliaji akiwa na uwezo wa kutengeneza nafasi na kumalizia mwenyewe. Sowah atatumika kwa nguvu na mwili wake mkubwa, huku Mwalimu akitarajiwa kutoa kasi na pressing ya kuwasumbua mabeki wa Malien.
KUNDI D NI KUNDI LA KIFO
Simba wako kwenye Kundi D sambamba na Esperance de Tunis, Stade de Malien, na Petro de Luanda. Ni kundi ambalo lina historia, ukubwa, uzoefu na ubabe. Kila timu imewahi kufika hatua kubwa Afrika.
Kwa Simba, mechi ya Jumapili ni zaidi ya kutafuta pointini mchezo wa kulinda heshima, kuamsha morali na kuonyesha kuwa bado ni moja ya klabu zenye malengo makubwa barani Afrika.



