BMT Yaishukia Simba Sc

584402558 18520670566071034 4697673469197920706 n

Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imeweka wazi msimamo wake kuhusu mabadiliko ya Katiba mpya ya Simba Sports Club, kwa kutoa maelekezo mazito yanayolenga kuimarisha mfumo wa uongozi, kuongeza uwazi katika uwekezaji na kulinda maslahi ya wanachama kama wamiliki halali wa klabu hiyo kongwe nchini.

Katika maelekezo hayo, BMT imesisitiza kuwa mchakato wa kuboresha Katiba ya Simba lazima uendane na misingi ya kisheria, utawala bora na uwiano wa uamuzi kati ya klabu na wawekezaji, ili kuondoa mkanganyiko ambao umekuwa ukizua mjadala kwa miaka kadhaa.

MWENYEKITI WA KLABU NDIE MWENYEKITI WA BODI YA WAKURUGENZI

Serikali imefafanua kuwa Katiba mpya lazima imtambue Mwenyekiti wa Simba SC kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Sports Club Company Limited. Msimamo huu umetolewa kwa kuzingatia ukweli kwamba wanachama kupitia klabu wanamiliki 51% ya hisa, wakati wawekezaji wanashikilia 49%.

Hivyo, Serikali imesema haiwezekani Mwenyekiti wa Klabu akawa chini ya kiongozi mwingine katika mfumo wa kampuni ilhali wanachama ndio wamiliki wakuu. Chini ya muundo huu, viongozi wote walio chini ya Bodi ya Wakurugenzi, wakiwemo watendaji wa kampuni, watawajibika kwa Mwenyekiti huyo kwa mujibu wa sheria, Katiba na kanuni za klabu.

MWENYEKITI NDIE KIONGOZI MKUU,AWE NA MAMLAKA YA KUITISHA MKUTANO MKUU

BMT Yaishukia Simba Sc-www.sportsleo.co.tz

Katika hatua nyingine, Serikali imeagiza Katiba mpya itaje kwa uwazi kuwa Mwenyekiti wa Simba SC ndiye Kiongozi Mkuu wa Chombo cha Utawala ndani ya Klabu.

Kwa msingi huo, atakuwa na mamlaka ya kuitisha mkutano mkuu wa wanachama, kwa kuwa mijadala inayofanyika katika mkutano huo kuhusu uanachama, maendeleo ya klabu na masuala ya kiutawala inaathiri moja kwa moja maslahi ya wanachama, ambao ndio kiini cha uwepo wa Simba SC kama klabu ya wanachama.

Serikali imesisitiza kuwa muundo huu unasaidia kupunguza mgongano wa madaraka uliowahi kujitokeza katika vipindi tofauti, ambapo baadhi ya mamlaka yalionekana kuhamia upande wa kampuni na kuiacha klabu inayomilikiwa na wanachama ikiwa na nguvu ndogo.

SERIKALI YATAKA NENO “MWEKEZAJI” LIBADILISHWE LIWE “WAWEKEZAJI”

Moja ya maeneo ambayo BMT imeitaka Simba kuyarekebisha ni matumizi ya neno “MWEKEZAJI.” Serikali imependekeza neno hilo liondolewe na badala yake litumike neno “WAWEKEZAJI”, likiwa na maana pana na shirikishi.

Serikali imesema ni muhimu Katiba kuonesha bayana kuwa uwekezaji ndani ya Simba hauna bwana mmoja, bali unapaswa kuruhusu uwepo wa zaidi ya mtu mmoja ili kuepusha udhibiti wa upande mmoja pekee.

Aidha, BMT imeagiza kuwa Baraza la Wadhamini, kwa niaba ya wanachama, ndio chombo pekee kinachopaswa kusaini mikataba ya uwekezaji na makubaliano yoyote ya kibiashara. Hatua hii inalenga kulinda maslahi ya wanachama, ambao mara nyingi hawajui undani wa mikataba iliyokuwa ikifanyika kati ya klabu na mfanyabiashara mmoja au wawili.

BMT Yaishukia Simba Sc-www.sportsleo.co.tz

WIGO MPYA WA UWEKEZAJI,MASLAHI YA WANACHAMA YAPEWE KIPAUMBELE

Kwa mujibu wa Serikali, marekebisho haya yote yanakusudia kupanua wigo wa uwekezaji ndani ya Simba SC bila kuhatarisha mali, hadhi na maslahi ya wanachama.

Serikali imesisitiza kuwa uwekezaji ni muhimu kwa maendeleo ya klabu, lakini lazima ufanyike katika mfumo mzuri, shirikishi, na unaoeleweka vizuri na wanachama. Hii ni pamoja na ulinzi wa mali na utambulisho wa klabu ili visitoweke mikononi mwa mwekezaji mmoja bila ridhaa ya wanaSimba wenyewe.

Kwa mtazamo wa BMT, mabadiliko haya yatasaidia kujenga Simba imara zaidi, yenye usimamizi thabiti, uwekezaji mpana na utawala unaofuata Katiba bila kuacha mianya ya migogoro kati ya wanachama na wawekezaji.

MCHAKATO WA KATIBA SASA KWENYE MKONDO MPYA

Baada ya maelekezo haya, jukumu kubwa sasa limebaki kwa kamati ya Katiba pamoja na uongozi wa Simba kuhakikisha mabadiliko haya yanajumuishwa ipasavyo na kuwasilishwa kwa wanachama kwa ajili ya kupitishwa.

Kile kilicho wazi ni kwamba Serikali inataka Simba iwe klabu ya kisasa, lakini pia iwe na mizizi imara katika umiliki wa wanachama.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks