“Hatuogopi, tuko tayari.”Pedro Afunguka

590247425 1413390880146839 4508791489872748264 n

Kocha Mkuu wa Yanga SC, Pedro Gonçalves, ameweka wazi kuwa kikosi chake kiko tayari kwa pambano lao la pili la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji JS Kabylie ya Algeria, licha ya mazingira magumu na presha kubwa inayotegemewa kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo. Kwa mujibu wa kocha huyo, hakuna kitakachowatikisa wala kuwatoa kwenye malengo yao, kwani akili na nguvu yao yote imewekwa kwenye mchezo huo muhimu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Pedro alisema mchezo wa kesho ni hadithi mpya tofauti kabisa na ile waliyoicheza jijini Zanzibar dhidi ya FAR Rabat ambapo Yanga ilishinda 1-0. Anasisitiza kuwa matokeo hayo tayari yamepita, na sasa wanaangalia namna ya kupata ushindi mwingine ugenini ili kujiimarisha kwenye michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

"Hatuogopi, tuko tayari.”Pedro Afunguka-www.sportsleo.co.tz

“Kesho ni mechi mpya, mechi tofauti kabisa. Kilichotokea kwenye mechi ya kwanza kimeshapita, akili yetu iko kwenye mchezo wa kesho,” alisema Pedro Gonçalves.

“Tunajua mazingira yatakavyokuwa na tuko tayari. Kelele na hamasa za mashabiki wao zinaweza kuwa nguvu kwao, lakini pia zinatupa nguvu sisi wachezaji wetu kujituma zaidi uwanjani. Tuna mpango wetu na ni muhimu kuusimamia kwa dakika zote.”

Kocha huyo ameongeza kuwa haoni sababu ya kuhofu presha ya mashabiki wa JS Kabylie kwa sababu soka ni mchezo wa ushindani, na mashabiki popote duniani huja kufurahia mchezo.

“Naamini mashabiki wa JS Kabylie kesho wanakuja kutazama mpira na sisi tuko hapa kwa ajili ya kucheza mpira,” alisisitiza.

Kwa upande wa wachezaji, kiungo mshambuliaji wa Yanga sc Mohamed Doumbia, ambaye amekuwa mmoja wa nguzo muhimu katika kikosi cha Yanga msimu huu, naye amesema kuwa amani ndani ya timu ni kubwa na hamasa ya mashabiki wa Algeria haitawatisha bali itawapa msukumo wa kupambana zaidi.

"Hatuogopi, tuko tayari.”Pedro Afunguka-www.sportsleo.cotz

“Hamasa ya mashabiki jukwaani ni kitu kizuri kwa kila mchezaji. Naamini kila mchezaji anapenda kucheza katika mazingira yaliyochangamka, hivyo tuko tayari kufuata kile ambacho mwalimu ametuelekeza kwenye mchezo wa kesho,” alisema Doumbia.

Akizungumzia mazingira ya Algeria, hasa hali ya hewa ambayo imekuwa ikitajwa kuwa baridi kali kuliko ilivyo Afrika Mashariki, Doumbia alisema wachezaji wa Yanga wameshaanza kuizoea na hawaoni kama itakuwa kikwazo kwao.

“Hali ya hewa hapa ni baridi lakini tuna kundi kubwa la wachezaji wenye uzoefu wa kucheza katika mazingira tofauti. Unapocheza Ligi ya Mabingwa ni lazima ujiandae na kila kitu kwenye akili yako,” aliongeza.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa wa ushindani mkali, hasa ikizingatiwa kuwa JS Kabylie wapo nyumbani na wanahitaji ushindi baada ya kupokea kipigo kizito cha 4-1 kutoka kwa Al Ahly katika mchezo wao uliopita. Kwa upande wa Yanga, ushindi wao wa 1-0 dhidi ya FAR Rabat visiwani Zanzibar umeipa timu hiyo ari na kujiamini kuelekea mchezo huu.

Mashabiki wa Yanga nchini Tanzania na wale waliopo Algeria wanaamini kuwa timu yao inaweza kupata matokeo mazuri, hasa kutokana na nidhamu na mpangilio wa kikosi chini ya kocha Gonçalves. Mchezo huu pia ni fursa kwa mabingwa hao wa Tanzania kuendelea kuonyesha ubora wao barani Afrika, ambako wamekuwa wakifanya vizuri zaidi katika miaka ya hivi karibuni.

Kadiri dakika zinavyosogea kuelekea mtanange huo wa usiku wa leo, mashabiki wa soka barani Afrika wanatarajia pambano la kuvutia baina ya timu mbili zenye historia na mashabiki wenye hamasa kubwa. Yanga wataingia wakiwa na malengo ya kuondoka na pointi tatu au angalau matokeo chanya yatakayowaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata.

Macho yote sasa yameelekezwa kwenye uwanja wa JS Kabylie, ambapo Yanga SC itapambana kusaka ushindi muhimu ugenini, ikiwa na morali kubwa na sauti ya kocha wao ikiwatia moyo .

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks