Simba Sc Yapoteza Alama Tatu Mali

Klabu ya Simba SC imejikuta ikiendelea kuandamwa na matokeo mabaya katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kukubali kichapo cha pili mfululizo kwa kufungwa mabao 2-1 na wenyeji wao, Stade Malien ya Mali, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa 26th of March Stadium mjini Bamako. Hili ni pigo jingine kwa Wekundu wa Msimbazi ambao msimu huu wameweka wazi dhamira ya kurejea kwenye ubora wao wa kimataifa, lakini hadi sasa mambo yanaonekana kwenda ndivyo sivyo.
Simba ilishuka dimbani ikiwa na kikosi chenye sura ya ushindani, wakiamini kwamba safari hii wangerejesha heshima baada ya matokeo ya awali kutoufurahisha umma wa mashabiki. Kocha Selemani Matola, aliyekuwa akisimamia mchezo huo, aliwaamini Yakub Seleman golini, Shomari Kapombe na Anthony Mligo pembeni, huku Rushine De Leuck na Wilson Nangu wakicheza kama mabeki wa kati. Kwenye kiungo cha ulinzi, Neo Maema na Naby Camara walitakiwa kuweka uwiano kati ya kushambulia na kukaba, wakisaidiana na Jean Charles Ahoua, Ellie Mpanzu na Joshua Mutale kwenye eneo la kati, huku Seleman Mwalimu akipewa jukumu la kutafuta mabao.
Kwa upande wa mchezo, Simba walianza kwa kasi na ndani ya sekunde 40 tu walipata nafasi ya wazi ambayo ilipaswa kuingiza bao la mapema. Mpira uliopigwa na Mpanzu ulienda kugonga mwamba, ukawakosesha bao ambalo lingeweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo. Baada ya tukio hilo, wenyeji Stade Malien walionekana kuamka na kutawala mchezo kwa kasi ya ajabu, wakitumia nguvu, spidi na mashambulizi ya kujenga taratibu.
Dakika ya 16, mashabiki wa Simba walijikuta kimya baada ya Thadeus Keng kumalizia mpira uliotokea kuzagaaa kwenye eneo la hatari na kuipatia Stade Malien bao la kwanza. Wenyeji hawakusita kuendelea kulisaka bao la pili, na juhudi zao zilizaa matunda kupitia kichwa cha Zoumana Simpara ambaye alionekana kuwachanganya mabeki wa Simba kila alipogusa mpira. Kutoka hapo, kasi ya wapinzani ilizidi kuwa kubwa kiasi cha kuacha uongozi wa benchi la benchi la Simba wakitikisa vichwa, hali iliyowafanya mashabiki waliokuwa uwanjani na nyumbani kutokuamini macho yao.
Kipindi cha pili kilianza na mabadiliko kwenye aina ya uchezaji wa Simba. Walionekana kurejea na ari mpya na dakika ya 53 Neo Maema akapiga shuti kali lililojaa mbinu na nidhamu ya kimataifa, na kuipatia Simba bao la kufutia machozi. Bao hilo liliwasha moto mpya, na Kocha Dimitar Pandev alifanya mabadiliko ya kuongeza nguvu za ushambuliaji. Jonathan Sowah aliingia kuchukua nafasi ya Seleman Mwalimu, wakati Maurice Abraham na Chamo Karabou walichukua nafasi za Mutale na Ahoua.
Simba ilianza kushambulia kwa nguvu, ikipoteza nafasi kadhaa za wazi zilizoweza kuwarejesha mchezoni. Katika dakika za hatari, Yakub Seleman alifanya kazi ya ziada kwa kuokoa mchomo wa penalti ambao ungeweza kuzima kabisa matumaini ya Simba. Hata hivyo, mambo yalizidi kuwa mabaya baada ya Naby Camara kupewa kadi nyekundu, jambo lililowafanya Simba wakamilishe mchezo wakiwa pungufu.
Licha ya jitihada za mwisho mwisho, dakika 90 zilipoisha, Simba walibeba kichapo kingine na kupoteza alama tatu muhimu katika safari yao ya kusaka nafasi ya kusonga mbele kwenye hatua ya makundi.
Baada ya mchezo, Meneja Mkuu wa Simba SC, Dimitar Pantev, alizungumza kwa hisia lakini pia kwa uwazi, akieleza kuwa timu imepambana lakini bahati haikuwa upande wao “Mashabiki wanayo haki ya kukasirika. Ni timu kubwa, ina matarajio makubwa, na mimi siwezi kujitetea. Ni kweli, tumefanya mazoezi bila baadhi ya wachezaji waliokuwa timu ya taifa, lakini bado hilo si kisingizio,” alisema Pantev.
Ameongeza kuwa miezi miwili aliyokaa ndani ya klabu hiyo haitoshi kutimiza malengo yote, lakini anaelewa kwamba katika timu kubwa kama Simba, hakutakuwa na muda wa kusubiri. Aliwataka mashabiki waendelee kuwa na subira, akiwahakikishia kwamba kikosi kitakuja na kiwango bora zaidi katika siku chache zijazo.
Kwa upande wa mashabiki, sauti zao zinazidi kupanda wakitaka mabadiliko ya haraka ndani ya timu yao. Lakini kwa mujibu wa Pantev na benchi la ufundi, msimu bado ni mrefu na bado kuna nafasi ya kurekebisha makosa, kurejesha imani na kupigania heshima ya klabu ndani na nje ya nchi.
Simba sasa wanasubiri mchezo wao unaofuata wakiwa na dhamira moja kurejesha fomu ya Msimbazi. Muda ndio utakaoamua kama maneno ya Pantev yataendana na kazi uwanjani huku ikizingatiwa kuwa itavaana na ES Tunis katika mchezo miwili mfululizo nyumbani na ugenini.



