Singida Black Stars Yapata Pointi ya Kwanza Cafcc

get 2

Singida Black Stars imeandika ukurasa wake wa kwanza kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) baada ya kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, mchezo uliopigwa kwenye dimba jipya la New Amaan Complex, Zanzibar. Huu ni mchezo uliokuwa na msisimko wa aina yake, ukitawaliwa na hisia, presha na ujasiri mkubwa kutoka kwa vijana wa Singida ambao walionyesha hawaji kufoka, licha ya kuwa na mzigo wa kutafuta pointi zao za kwanza kwenye michuano hiyo.

Mashabiki waliofurika New Amaan walishuhudia dakika 90 zilizojaa shambulizi kwa shambulizi, huku Singida wakionesha dhamira ya kuipambania bendera ya Tanzania kwa nguvu zote. Ingawa Stellies walionekana kuingia na kujiamini zaidi kutokana na rekodi yao, haikuwazuia vijana wa kocha wao kusimama imara na kuonesha mpira wa kasi, nidhamu na upambanaji wa hali ya juu.

Dakika ya 52 ndiyo iliwakosesha Singida utulivu baada ya Langelihle Phili kuiandika Stellenbosch bao la kuongoza. Bao hilo lilikuwa pigo kwa mashabiki waliokuwa wakishangilia kila ukabaji na kila shambulizi, lakini halikukatisha tamaa kikosi cha nyumbani. Baada ya bao hilo, Stellenbosch walijaribu kupunguza kasi ya mchezo huku wakitegemea mashambulizi ya kushtukiza, lakini Singida hawakuruhusu wazunguke kwa uhuru.

Singida Black Stars Yapata Pointi ya Kwanza Cafcc-www.sportsleo.co.tz

Katika dakika za mwisho kuelekea tamati, Singida iliongeza kasi hadi kufanya shambulizi moja baada ya jingine kuelekea lango la wageni. Mashambulizi haya yakazalisha presha kubwa ambayo ilisababisha Stellies kufanya makosa kwenye eneo la hatari. Dakika ya 90+1 ndipo tukio lililowainua mashabiki wote lilipotokea penalti kwa Singida Black Stars!

Jukumu la kupiga likamwangukia kiungo mahiri, Marouf Tchakei, ambaye alisimama akiwa mtulivu kana kwamba anapiga penalti kwenye mazoezi. Mashabiki walikata shoti, baadhi wakiufunika uso kwa mikono, wengine wakisimama juu ya viti vyao. Tchakei akapiga kwa ustadi mkubwa, akamtuma kipa upande tofauti na kuandika bao lililorejesha tumaini na kulipua shangwe New Amaan. Bao lile lilikuwa zaidi ya alama  lilikuwa ujumbe kuwa Singida haiishi kwa kubahatisha, bali inapigana mpaka sekunde ya mwisho.

Baada ya bao hilo, mchezo ulizidi kuchemka kwa dakika chache zilizobaki, Singida wakisaka bao la pili kwa nguvu zote. Hata hivyo, muda haukuwa rafiki, na refa alipolia filimbi ya mwisho, matokeo yakawa Singida Black Stars 1-1 Stellenbosch. Sare hii imeifanya Singida kupata pointi yake ya kwanza kwenye hatua ya makundi ya CAFCC, jambo lililowapa mashabiki faraja na matumaini mapya kuelekea mechi zijazo.

Singida Black Stars Yapata Pointi ya Kwanza Cafcc-www.sportsleo.co.tz

Kwa sasa, Singida inashika nafasi ya nne kwenye Kundi C ikiwa na pointi 1, nyuma ya Stellenbosch wanaoongoza kwa pointi 4, Otoho d’Oyo walio na 3, pamoja na CR Belouizdad wenye pointi 3 pia. Pamoja na kuwa mwisho kwa sasa, kiwango walichoonesha dhidi ya Stellenbosch kimetoa taswira kuwa kundi bado lipo wazi, na lolote linaweza kutokea katika michezo ijayo.

Kocha wa Singida Black Stars Miguel Gamond alionekana kufurahishwa na uchezaji wa wachezaji wake, akisema kuwa walistahili hata zaidi ya pointi moja. Mashabiki pia waliwaaga wachezaji wao kwa makofi na kuwashangilia kwa kusawazisha,wakiamini kwamba kama timu itaendelea kucheza kwa ari ile ile, basi ina nafasi ya kupenya katika kundi gumu kama hilo.

Kwa mtindo waliouonyesha, Singida Black Stars imeonyesha kuwa safari yao ya michuano ya Afrika haiko kwenye maneno bali vitendo. Sare yao ya kwanza imezua maswali kwa wapinzani wao na kutoa jibu moja kwa mashabiki waoSingida haiji kutalii katika CAFCC, inakuja kupigania heshima ya Tanzania

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks