Singida BS Yaifuata Cr Belouzdad

Kikosi cha Singida BS kimeandika sura mpya katika historia yake ya ushiriki wa michuano ya kimataifa baada ya kuondoka mapema alfajiri ya leo, Novemba 18, 2025, kuelekea Algeria kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) dhidi ya CR Belouizdad.
Safari hiyo imeacha gumzo kubwa, si tu kwa mashabiki wa Singida BS, bali hata kwa wadau wa soka nchini kutokana na maamuzi ya dakika za mwisho yaliyofanywa na uongozi wa klabu hiyo.
Wakiwa wamepania kuhakikisha hawafanyi makosa katika mechi yao ya ufunguzi, Singida BS waliondoka Dar es Salaam kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakipitia Istanbul, Uturuki kabla ya kuelekea moja kwa moja jijini Algiers, Algeria, kupitia ndege ya Turkish Airlines. Hata hivyo, kilichoibua maswali mengi ni taarifa kwamba awali safari hiyo ilikuwa imepangwa kufanyika kesho, Novemba 19 lakini kikosi kiliamua “kubadili gia wakiwa angani,” hatua inayoonyesha dhamira ya kuhakikisha maandalizi yanakuwa ya kiwango cha juu kabisa.
Kwa wapenda soka wanaoifuatilia Singida BS, kitendo cha timu kuondoka mapema hakiwezi kuwa jambo la kushangaza sana, maana uongozi wa klabu hiyo umejenga utamaduni wa kufanya maandalizi mazito wanapokwenda kwenye michezo mikubwa. Tangu walipoingia kwenye ramani ya soka la kimataifa, Singida BS wamekuwa wakitengeneza taswira ya klabu yenye umakini, nidhamu na ubora wa juu, vitu ambavyo vinawafanya waonekane kama mmoja wa wawakilishi wanaoweza kwenda mbali katika michuano ya CAF mwaka huu.
Safari ya kuelekea Algeria imekuja wakati ambao morali ndani ya kikosi iko juu, hasa baada ya kocha mkuu na benchi lake la ufundi kufanya maandalizi ya kina kwa wiki kadhaa, wakijua wazi kwamba mchezo dhidi ya CR Belouizdad si mzaha. Klabu hiyo ya Algeria imewahi kushiriki michuano ya kimataifa mara kwa mara na ina wachezaji waliokomaa kisoka lakini kwa upande wa Singida BS, jambo hilo limeonekana kuongeza hamasa badala ya uoga.
Hali hewa ya jiji la Algiers pia imechukuliwa kwa uzito na benchi la ufundi, kwani wakati huu wa mwaka hali ya baridi huwa kali, tofauti na hali ya joto la Dar es Salaam. Ndiyo maana uamuzi wa kuwasili mapema unalenga kutoa muda wa kutosha kwa wachezaji kuizoea mazingira mapya, kurekebisha miili yao kutokana na tofauti ya muda na hali ya hewa, pamoja na kufanya mazoezi ya mwisho kwenye viwanja vitakavyotolewa na wenyeji.
Mashabiki wa Singida BS nao wameonesha hamasa ya hali ya juu kupitia mitandao ya kijamii, wakituma salamu za heri kwa wachezaji wao huku wengine wakiwataka “kuilipua” Algeria na kuanza hatua ya makundi kwa kishindo. Wapo waliokwenda mbali zaidi na kusema kwamba huu ndio mwaka ambao Tanzania inaweza kuandika rekodi mpya kwenye michuano ya CAF kupitia klabu hiyo inayoonekana kuwa na mipango imara na uwekezaji mkubwa.
Uongozi wa klabu kupitia msemaji wao umeeleza kuwa wanachukulia mchezo wa Novemba 22 kama fursa ya kuonyesha ubora wao barani Afrika, huku akisisitiza kuwa timu imekwenda Algeria ikijua wanakabiliwa na kazi ngumu lakini inayowezekana. “Tunajua Belouizdad ni timu yenye uzoefu, lakini pia tunajua ubora wetu. Tumejipanga, tumewahi, na tutafanya kila linalowezekana kuanza kwa ushindi,” alisema kwa kujiamini.
Mchezo huo, ambao utachezwa jijini Algiers, utakuwa kipimo cha kwanza cha ubora wa Singida BS katika hatua ya makundi,Bila shaka mashabiki wengi wa soka nchini watakuwa wakitazama kwa jicho la pekee, si tu kuona namna Singida BS wanavyoanza safari yao ya makundi, bali pia kuona kama Tanzania inaweza kuwa na mwakilishi mwingine wa kutisha barani Afrika baada ya mafanikio ya miaka ya karibuni kutoka Simba na Yanga.
Kwa sasa macho yote yako Algeria ambapo Singida BS wanakwenda kutafuta alama tatu muhimu, lakini pia heshima na hadhi ya soka la Tanzania. Ni safari iliyobeba matumaini mazito. Na kama walivyobadili gia angani, basi ni wazi kabisa kuwa wanatafuta kuandika historia kwa namna isiyo ya kawaida. Hii ndiyo Singida BS mpya, yenye njaa ya mafanikio na inayotaka kuacha alama barani Afrika.

