Camara Afanyiwa Upasuaji Morocco

Golikipa wa Simba SC, Moussa Camara, hatimaye amepelekwa kwenye meza ya upasuaji nchini Morocco kufuatia jeraha la goti lililokuwa likimtesa kwa muda sasa, na kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka ndani ya klabu hiyo, upasuaji huo umefanikiwa kwa asilimia mia moja.
Operesheni hiyo ilifanyika Jumanne, Novemba 18, 2025, na madaktari wamethibitisha kuwa mchezaji huyo sasa yuko katika uangalizi maalumu akisubiri kuanza hatua ya tiba ya kurejesha nguvu (rehabilitation).
Kwa mujibu wa chanzo kinachofahaminika na Sportsleo Camara sasa anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa takribani wiki nane hadi kumi, muda ambao unaweza kuwa mrefu zaidi endapo atachelewa kurudi katika kiwango cha juu,Hata hivyo, benchi la ufundi la Simba pamoja na madaktari wao wameeleza kuwa wana imani kubwa kipa huyo ataweza kurudi akiwa imara zaidi, kwani upasuaji umefanyika kwa viwango vya kimataifa katika moja ya vituo bora vya tiba za michezo nchini Morocco.
ILIVYOTOKEA MPAKA AKAUMIA
Chanzo cha jeraha la Camara kimetokana na tukio lililotokea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nzingizini Hotspurs ya Comoro, mechi iliyochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Katika dakika za kipindi cha pili, Camara alijikuta akishtuka baada ya kugongana na mshambuliaji wa timu pinzani wakati akijaribu kuokoa mpira hatari.
Watazamaji walioshuhudia tukio hilo waliona jinsi alivyoshika goti lake la kushoto huku akionekana kutokuwa na uwezo wa kuendelea na mchezo. Dakika chache baadaye, benchi la ufundi lililazimika kumpumzisha na nafasi yake kuchukuliwa na Yakub Seleman, ambaye alimaliza mchezo huo hadi mwisho.
SIMBA YATULIZA PRESHA YA MASHABIKI
Habari za upasuaji huo zimepokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa Simba, huku baadhi wakihofia pengo watakaloachwa na Camara ambaye msimu huu ameonekana kuwa mhimili kwenye safu ya ulinzi wa timu hiyo.
Hata hivyo, uongozi wa Simba umejitokeza kutuliza mashabiki kwa kueleza kuwa mipango madhubuti imewekwa kuhakikisha timu haiyumbi wakati kipa wao namba moja akipona. Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo Ahmed Ally aliliambia gazeti letu kuwa wana imani na makipa waliopo kikosini na kwamba benchi la ufundi litazidi kufanya mabadiliko ya kimkakati kuhakikisha hali ya ushindani kwenye kikosi inabaki palepale.
“Hatuwezi kuficha, kumkosa Camara ni pigo, lakini soka ni mchezo wa timu. Wachezaji wengine wako tayari kupambana kuhakikisha hatupotezi mwelekeo,” alisema.
BENCHI LA UFUNDI LAMPOKEA UJUMBE WA MATUMAINI
Meneja mkuu wa Simba Sc Dimitri Pandev naye ametoa ujumbe mzito wa matumaini kwa Camara huku akimtakia uponaji wa haraka. Amesema kuwa licha ya changamoto za kimwili, wachezaji wengi huwa wanarudi wakiwa bora zaidi baada ya upasuaji endapo watapita kwenye hatua sahihi za tiba.
“Camara ni mchezaji mwenye nidhamu kubwa, hana kiburi katika mazoezi na anafuata maelekezo ya kitabibu bila kupinga. Tunaamini atarudi haraka na kutupa msaada mkubwa kama kawaida yake,” alisema kocha huyo.
MASHABIKI WAMTUPIA SALAMU ZA POLE
Katika mitandao ya kijamii, mashabiki wa Simba wamekuwa wakimtumia ujumbe wa faraja Camara, wengi wao wakimtakia kurejea kwa nguvu zaidi. Baadhi wameandika kuwa jeraha ni sehemu ya mchezo na kwamba wanatarajia kumuona tena akisimama langoni kwa utulivu wake wa kawaida.
Kwa sasa, Camara atabaki Morocco kwa siku chache kabla ya kurejea Dar es Salaam kuendelea na hatua za mwisho za tiba na mazoezi ya utimamu wa mwili chini ya uangalizi wa wataalamu wa Simba SC.


