Kamwe Awasha Moto Caf

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ali Kamwe, amewasha moto wa mashabiki baada ya kutamka kuwa mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FAR Rabat ya Morocco utakuwa na uzito wa kipekee ambao haujawahi kuonekana katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambapo mchezo huo utapigwa Novemba 22, 2025, na tayari taharuki, msisimko na presha vimetanda pande zote za visiwa.
Akizungumza kwa kujiamini, Kamwe amesema mechi hiyo itakuwa “zaidi ya mechi”, akitamba kuwa ni moja ya michezo inayozungumzwa zaidi barani Afrika kwa sasa kutokana na ukubwa wa timu zinazokutana, rekodi zao na ukubwa wa mashabiki wanaoifuatilia. Amekiri kuwa Yanga inaenda kupambana na moja ya klabu imara zaidi Kaskazini mwa Afrika, lakini bado anaamini kuwa pointi tatu zinabaki kwa Wananchi.
“Mechi ya Yanga dhidi ya FAR Rabat ndiyo mechi kubwa zaidi kuwahi kuchezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex,” alisisitiza Kamwe. “Huu ndio mchezo unaozungumzwa zaidi barani Afrika kwa sasa. Usiifananishe na mechi nyingine yoyote iliyowahi kuchezwa Aman Complex. Hakuna mtu anayetaka kusimuliwa mchezo huu, kila mtu anatamani uwepo uwanjani.”
Kauli hiyo imezidi kuchochea hamasa kwa mashabiki wa Yanga Sc walioko Zanzibar na Tanzania Bara kwa ujumla, ambao kwa wiki mbili mfululizo wamekuwa wakijazana kwenye mitandao, maduka ya jezi na vijiwe vya michezo wakiongelea pambano hilo. Wengi wanasema wamekosa usingizi tangu ratiba iwekwe wazi.
Kamwe amesema moja ya sababu inayofanya mechi hii kuwa na mvuto wa kipekee ni ukweli kwamba mataifa mbalimbali yatamiminika Zanzibar kushuhudia mchezo huo. Amedai kambi ya waandishi wa habari wa Morocco, Algeria, Misri, Afrika Kusini na hata baadhi ya wachambuzi kutoka Ulaya wanatarajiwa kufika Amaan Complex kuripoti tukio hilo. “Hii ni mechi ya dunia, si ya kawaida,” amesema.
Akijibu maswali ya mashabiki ambao wamekuwa wakimfuata mitandaoni kuuliza kuhusu burudani ndani ya uwanja, Kamwe amesisitiza kuwa watu hawataki tena kusimuliwa namna ambayo Pacome Zouzoua atakavyowatesa Waarabu wa Morocco. “Mashabiki wanataka kumuona Pacome mwenyewe, live, akipiga chenga na pasi za macho,” alisema. “Huu ni wakati ambao kila shabiki wa Yanga anatamani kushuhudia historia ikiandikwa.”
Hata hivyo, sambamba na kuongeza hamasa, Kamwe ameendelea kutoa angalizo muhimu nunua tiketi mapema. Ametahadharisha kuwa New Amaan Complex ni uwanja wenye uwezo mdogo ukilinganisha na kasi ya mashabiki wa Yanga, hivyo kuna uwezekano mkubwa uwanja kujaa kabla hata ya siku ya mchezo kufika.
“Tayari tiketi zimeanza kuuzwa leo kwenye vituo mbalimbali na kwa njia ya mtandao. Kwa wale mlio Zanzibar, kadi zenu mtatumia zilezile. Ukipoteza kadi, kesho nje ya uwanja kutakuwa na eneo rasmi la kupata kadi mpya. Jitokeze mapema, usikose burudani hii kubwa Afrika,” ameeleza.
Kwa upande mwingine, kikosi cha Yanga tayari kimesafiri kuelekea Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mwisho. Hii imeifanya hali kuwa ya aina yake kwani mashabiki wameanza kuifuata timu kila inakopita, wengine wakipiga picha, wengine wakipeperusha bendera na wengine wakitaja matokeo wanayoyatarajia.
Hadi sasa, Yanga wanapigiwa hesabu kubwa ya kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi kutokana na usajili wao wa kiwango cha juu, kocha aliyejidhihirisha barani Afrika, pamoja na muunganiko bora wa kikosi ambacho kimekuwa imara kwenye mashindano ya CAF kwa misimu mitatu mfululizo.
Mashabiki katika mitaa ya Kariakoo, Kigamboni, Magomeni, Kinondoni na maeneo ya Pwani tayari wameanza kupanga safari za mapema kuelekea Zanzibar wengine wakipanda boti, wengine ndege, na baadhi wakipanga kutimka kufika mapema siku moja kabla ya mchezo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya benchi la ufundi, Yanga ipo na morali ya hali ya juu, wachezaji wako fiti na kocha anaamini kikosi kitafanya kazi kubwa dhidi ya Waarabu. Hali hii, ikijumuishwa na maneno ya Kamwe, imeongeza moto ambao unalifanya pambano hili kuwa tukio la kihistoria ambalo litakumbukwa kwa miaka mingi ijayo.



