Yanga Sc Yaichapa Simba Sc 1-0, Yatwaa Ngao Ya Jamii

Yanga Sc imeanza msimu mpya kwa kishindo! Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara wameonyesha kuwa bado wako kwenye kasi ileile ya ubabe baada ya kuwachapa watani wao wa jadi Simba Sc kwa bao 1-0 na kutwaa Ngao ya Jamii kwa msimu wa 2025/26.
Katika mechi hiyo ya kuvutia iliyopigwa mbele ya mashabiki kibao kwenye Uwanja wa Taifa, bao pekee la Pacome Pedoh Zouzoua dakika ya 54 ya mchezo lilitosha kuihakikishia Yanga Sc taji hilo muhimu la kufungua msimu lakini kilichoweka alama kubwa zaidi ni ubora wa kipa Djigui Diarra na mipango kabambe ya kiungo mkabaji, Aziz Andambwile.
Diarra Si Binadamu wa Kawaida
Kama kuna mchezaji aliyeamua kuivaa jezi ya Yanga Sc kishujaa kwenye mechi hii, basi ni kipa raia wa Mali, Djigui Diarra. Alikuwa kizingiti kizito kwa washambuliaji wa Simba, hasa katika dakika za lala salama ambapo Simba walitafuta bao la kusawazisha kwa udi na uvumba.
Kipindi cha kwanza mshambuliaji wa Simba Sc Kibu Dennis alipata nafasi ya kukutana nae uso kwa uso lakini kipa huyo aliokoa mpira huo huku Shomari Kapombe nae alipiga shuti kali ndani ya mita 18 lakini Diarra aliruka kama tai na kuokoa kwa ustadi mkubwa. Ilikuwa ni moja ya ‘saves’ bora kabisa kuonekana kwenye mechi za Ngao ya Jamii kwa miaka ya karibuni.
Si tu aliokoa michomo ya hatari, bali aliwasiliana vyema na mabeki wake, akiongoza safu ya ulinzi kwa ustadi na utulivu mkubwa. Bila shaka, Diarra ameonyesha kuwa bado ni nguzo kuu ya mafanikio ya Yanga.
AZIZ ANDAMBWILE – Ukuta Usiopenyeka Kirahisi
Kwa upande wa viungo mashabiki wengi walitarajia kuwa kocha Roman Folz angeanza na Balla Mousa Conte ili kuibeba Yanga kama kawaida, lakini katika mechi hii, jicho la mtaalamu lilimfuata kiungo mkabaji Aziz Andambwile,ambaye alicheza kama chuma akiwazuia viungo washambuliaji wa klabu ya Simba Sc wakiongozwa na Ellie Mpanzu.
Andambwile alidhibiti katikati ya uwanja kwa umahiri wa hali ya juu, akivunja mashambulizi ya Simba kabla hayajakomaa na kusambaza mipira kwa usahihi mkubwa. Uwepo wake ulifanya kina Allasane Kante na Jean Charles Ahoua washindwe kabisa kutawala sehemu ya kiungo kama walivyozoea.
Uchezaji wake umetuma ujumbe kuwa Yanga wamepata mchezaji mwingine wa daraja la juu ambaye anaweza kuziba pengo la Khalid Aucho aliyekuwa tegemeo kwenye nafasi hiyo miaka ya nyuma.
Yanga Sc Sasa Iko Tayari kwa Ligi
Ushindi huu dhidi ya Simba si tu umetwaa Ngao ya Jamii, bali umetuma ujumbe mzito kwa timu zote za Ligi Kuu. Yanga imeonyesha kuwa haikuridhika na mafanikio ya misimu miwili iliyopita na bado wanataka zaidi ambapo kikosi hicho kimesheheni mastaa wa kila iana kwa sasa kuanzia eneo la ulinzi mpaka ushambuliaji.
Kocha mkuu wa Yanga Sc Roman Folz, amesema baada ya mechi kuwa amefurahishwa na nidhamu ya wachezaji wake na jinsi walivyotekeleza maelekezo ya kiufundi.
“Tulijua Simba ni timu kubwa, lakini tulijipanga vizuri, hasa kwenye ukabaji na matumizi ya nafasi. Diarra na Andambwile walicheza kwa kiwango cha juu sana na pia timu kwa ujumla,” alisema Folz.
Simba Sc Sasa Wamefungwa Mara ya Sita Mfululizo
Kwa upande wa Simba sasa wamefungwa kwa mara ya sita mfululizo na Yanga sc huku wakiwa hawajapata bao lolote katika michezo minne mfululizo mpaka sasa yote ikiwa chini ya kocha Fadlu Davies ambaye sasa inabidi afanye tathmini ya kutosha kuhusu mbinu zake dhidi ya Yanga sc.

Hata hivyo katika mchezo huu licha ya kupoteza mechi, bado walionyesha dalili ya timu nzuri, hasa kipindi cha kwanza walipokua wanajenga mashambulizi mazuri na hata walipofungwa kipindi cha pili bado walipojaribu kurejea mchezoni. Hata hivyo, tatizo la mwisho wa umaliziaji bado linaonekana — kitu ambacho kocha Fadlu atalazimika kukifanyia kazi haraka kabla ya msimu kuanza rasmi hasa Kibu Dennis ambaye mara kadhaa alikosa nafasi akiwa yeye na kipa Djigui Diarra.
Mwisho wa Mchezo,Yanga Sc 1-0 Simba
Mfungaji: Pacome Zouzoua (Yanga) – Dakika ya 54
Mchezaji waliokua Bora: Djigui Diarra (Yanga SC),Aziz Andambwile,Rushine De Look (Simba Sc)
Kadi: Mechi ilikuwa ya kiungwana – hakuna kadi nyekundu, kadi za manjano chache tu 5 kwa Simba Sc na 4 kwa Yanga sc
Mashabiki Wanasemaji?
Mashabiki wa Yanga wamefurika mitandao ya kijamii kusifu kikosi chao huku wengi wakimtaja Diarra kama “mkombozi wa Jangwani.” Wengine wamesema ushindi huu ni kama “kuanza msimu na pasipoti ya ubingwa mkononi.”
Kama Yanga wataendeleza kiwango hiki, basi msimu huu unaweza kuwa wa kihistoria zaidi kuliko ilivyokuwa misimu miwili iliyopita.

