Cameroon,Ivory Coast Watoa Sare Afcon 2025

b25l2rw1128

Timu ya Taifa ya Cameroon na mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika, Ivory Coast, wamelazimishana sare ya bao 1-1 katika mchezo mkali wa Kundi F uliochezwa jijini Marrakesh, Morocco, kwenye michuano ya AFCON 2025. Baada ya dakika 90 za upinzani wa hali ya juu, hakuna timu iliyoweza kupata bao la ushindi katika pambano lililojaa kasi, mbinu na hatari langoni.

Bao la Junior Tchamadeu katikati ya kipindi cha pili, likisaidiwa na mkwaju uliogonga mchezaji wa Ivory Coast na kubadili mwelekeo, liliisadia Cameroon kusawazisha baada ya Ivory Coast kuwa mbele kwa bao la kifahari lililofungwa na Amad Diallo. Mechi hiyo ilikuwa na kila kitu ikiwemo ubora wa kiufundi, nguvu ya mwili na msisimko mkubwa uliowashika mashabiki hadi filimbi ya mwisho.

b25l2rw1128

Dakika za mwanzo zilianza kwa tahadhari kubwa kutoka pande zote mbili, kila timu ikijaribu kusoma mbinu za mpinzani wake kabla ya kushambulia kwa nguvu. Cameroon walionekana kujiamini zaidi katika dakika za awali, wakitumia vyema mipira ya pembeni na mipira ya juu.

Dakika ya 20, Indomitable Lions walikuwa karibu kuvunja ukimya baada ya Christian Kofane kuruka juu zaidi kuupiga mpira wa kichwa uliotoka upande wa kushoto. Hata hivyo, mpira huo uligonga mwamba wa juu wa lango na kuacha mashabiki wa Cameroon wakishika vichwa kwa masikitiko.

Ivory Coast walionekana kuongeza kasi kadri muda ulivyokwenda, wakitumia uzoefu wao kama mabingwa watetezi. Dakika chache kabla ya mapumziko, nahodha Franck Kessié aliamini ameipa timu yake bao la kuongoza baada ya kupiga shuti la karibu kufuatia mpira uliokuwa umesalia ndani ya boksi. Shangwe za mashabiki wa Ivory Coast zilikatizwa ghafla baada ya mwamuzi, kwa msaada wa waamuzi wasaidizi, kuamuru kuwa kulikuwa na mtego wa kuotea katika pasi ya awali kutoka kwa Vakoun Issouf Bayo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ya juu, huku soka la kushambuliana likitawala dakika za mwanzo. Timu zote zilionekana kurekebisha mbinu zao, zikishambulia kwa haraka na kubadilishana mashambulizi ya hatari.

Dakika za mwanzo baada ya mapumziko, Amad Diallo aliibuka kuwa shujaa wa Ivory Coast kwa kuonyesha kipaji cha hali ya juu. Mshambuliaji huyo wa Manchester United aliupokea mpira upande wa kulia, akakata kuelekea ndani kwa mguu wake wa kushoto na kupiga shuti la mviringo lililomshinda kipa Devis Epassy, na kuipa Ivory Coast bao la kuongoza lililozua shangwe kubwa uwanjani.

b25l2ag1610

Hata hivyo, Cameroon hawakukaa nyuma kwa muda mrefu. Dakika tano tu baada ya bao hilo, Junior Tchamadeu alijikuta ndani ya boksi na kupiga shuti lililogonga mchezaji wa Ivory Coast, Ghislain Konan, na kubadili mwelekeo kabla ya kumhadaa kipa na kuingia wavuni. Bao hilo liliwarejesha Cameroon kwenye mchezo na kuufanya uwanja kulipuka kwa shangwe.

Baada ya kusawazishwa, mchezo uligeuka kuwa wa presha kubwa huku kila timu ikisaka bao la ushindi. Cameroon walimtegemea sana Bryan Mbeumo, lakini ulinzi wa Ivory Coast ulikuwa imara na wenye nidhamu. Jaribio lake bora lilitokana na mpira wa adhabu uliopigwa kutoka nje kidogo ya boksi, lakini mpira huo ulipita karibu na lango bila kuleta madhara.

Kwa upande wa Ivory Coast, walijaribu kutumia kasi ya Diallo na mipira ya kati ya Kessié kutengeneza nafasi, lakini safu ya ulinzi ya Cameroon ilisimama imara na kuzuia mashambulizi mengi hatari.

Dakika za lala salama zilishuhudia presha kutoka pande zote mbili, huku kila timu ikifanya mabadiliko ya kimkakati kutafuta bao la ushindi. Licha ya jitihada hizo, hakuna timu iliyoweza kuvunja ukuta wa ulinzi wa mpinzani wake, na mchezo ukaisha kwa sare ya haki kwa pande zote.

Matokeo hayo yameziacha Cameroon na Ivory Coast zikiwa na pointi nne kila moja katika Kundi F, huku zikifungana pia kwa idadi ya mabao yaliyofungwa na kufungwa. Hali hiyo imeufanya mchezo wa mwisho wa kundi kuwa wa maamuzi makubwa.

Sasa macho yataelekezwa kwenye raundi ya mwisho ya michezo ya kundi itakayochezwa mkesha wa Mwaka Mpya. Cameroon wanasafiri kurejea Agadir kwa ajili ya mchezo dhidi ya Msumbiji, huku mabingwa watetezi Ivory Coast wakibaki Marrakesh kumenyana na Gabon ambao tayari wameondolewa kwenye mashindano.

Kwa mwenendo huu, mashabiki wa soka barani Afrika wanatarajia michezo ya mwisho ya makundi itakuwa ya moto zaidi, huku kila timu ikipambana kuhakikisha inatinga hatua ya 16 bora ya AFCON 2025.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks