Mahrez Aipa Algeria Tiketi 16 Bora

Nahodha Riyad Mahrez ameibuka shujaa kwa Algeria baada ya kufunga bao pekee la penalti lililoihakikishia timu hiyo ushindi wa thamani wa mabao 1-0 dhidi ya Burkina Faso, matokeo yaliyothibitisha kufuzu kwa Les Fennecs kwenda hatua ya 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 linaloendelea nchini Morocco.
Kwa ushindi huo, Algeria imejiimarisha kileleni mwa Kundi E kwa pointi sita baada ya kushinda mechi mbili mfululizo. Burkina Faso wamesalia nafasi ya pili wakiwa na pointi tatu, sawa na Sudan ambao mapema waliifunga Equatorial Guinea kwa bao 1-0. Hali hiyo imeufanya mchezo wa mwisho wa kundi kuwa wa maamuzi makubwa kwa tiketi ya pili ya kufuzu.

Mchezo huo ulikuwa mgumu, wenye nguvu nyingi na mapambano ya kimwili tangu dakika za mwanzo, hali iliyolazimisha Algeria kufanya mabadiliko ya mapema. Dakika ya 13, beki Juan Hadjam alilazimika kuondolewa uwanjani kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya changamoto nzito kutoka kwa Gustavo Sangaré wa Burkina Faso. Kocha Vladimir Petković alilazimika kumuingiza mshambuliaji Baghdad Bounedjah mapema kuliko ilivyopangwa.
Mchezo uliendelea kwa kasi kubwa, huku kila timu ikijaribu kudhibiti eneo la kati. Lakini nguvu hizo hizo ndizo zilizoigharimu Burkina Faso baada ya Rayan Aït-Nouri kuangushwa ndani ya eneo la hatari dakika ya 23 na beki Ismahila Ouedraogo. Mwamuzi hakuwa na shaka kuashiria penalti, uamuzi uliowapa Algeria nafasi ya dhahabu kuchukua uongozi.
Nahodha Mahrez alisimama kwenye mkwaju wa penalti kwa utulivu mkubwa, akimpiga kipa mwelekeo tofauti na kuupiga mpira wavuni, na kuipa Algeria bao la mapema lililodhibiti mwelekeo wa mchezo. Bao hilo liliongeza kujiamini kwa Les Fennecs huku Burkina Faso wakilazimika kuongeza mashambulizi.
Algeria walikaribia kuongeza bao la pili kabla ya mapumziko, lakini Mohamed Amoura alishindwa kuitumia pasi safi ya Mahrez baada ya shuti lake la karibu kuokolewa kwa ustadi na kipa wa Burkina Faso, Kouakou Koffi. Hata hivyo, kipindi cha kwanza kilimalizika Algeria wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ileile, Algeria wakionekana kutaka kumaliza kazi mapema. Wachezaji wa Petković walitengeneza nafasi kadhaa kupitia Ibrahim Maza na Aït-Nouri, lakini Koffi aliendelea kuwa mwiba kwa kuokoa mashuti mawili hatari yaliyokuwa karibu kuongeza majonzi kwa Burkina Faso.
Burkina Faso nao hawakuwa nyuma, wakijaribu kusawazisha kupitia mashambulizi ya kushtukiza. Nafasi yao bora ilikuja kupitia mchezaji aliyeingia kipindi cha pili, Georgi Minoungou, ambaye alipiga shuti la mzunguko lililopita juu kidogo ya mwamba wa juu wa lango, na kuacha mashabiki wakishika pumzi.
Kadiri dakika zilivyokwenda, presha iliongezeka kwa Burkina Faso wakisaka bao la kusawazisha, lakini Algeria walionyesha nidhamu kubwa ya ulinzi, wakiongozwa na safu ya nyuma iliyosimama imara na kuondoa hatari nyingi. Licha ya jitihada za mwisho za Burkina Faso, filimbi ya mwisho ilikuta Algeria wakilinda ushindi wao mwembamba lakini muhimu.
Matokeo hayo yanamaanisha Algeria sasa wataingia katika mchezo wa mwisho wa kundi wakiwa tayari wamefuzu, ambapo watakutana na Equatorial Guinea ambao tayari wameondolewa kwenye mashindano. Kwa upande mwingine, Burkina Faso watavaana na Sudan katika pambano la moto litakaloamua timu itakayopata tiketi ya pili ya moja kwa moja kwenda hatua ya mtoano. Michezo hiyo miwili itachezwa mkesha wa Mwaka Mpya.
Mchezaji Bora wa Mechi (MOM), Ibrahim Maza wa Algeria, alisema ushindi huo ulikuwa matokeo ya kazi ya pamoja “Leo ushindi umetokana na timu nzima. Kila mmoja alicheza vizuri na jambo muhimu zaidi lilikuwa kushinda mechi. Lengo letu lilikuwa kufuzu, siyo tuzo binafsi. Sasa tumefuzu rasmi na tunafurahia kazi tuliyofanya.”Alisema staa huyo kwa kujiamini.
Maza aliongeza kuwa walijua mchezo ungekuwa mgumu kutokana na nguvu za Burkina Faso “Tulijua watakuwa wagumu kwenye mapambano ya mwili, kwa hiyo nasi tulihitaji kuwa imara kwenye mipambano, na nadhani tulifanikiwa.”Alimalizia kusema
Kocha wa Burkina Faso, Brama Traore, alisema penalti ndiyo ilibadili mwelekeo wa mchezo “Tulitaka kushinda mechi hii. Kucheza dhidi ya Algeria siku zote ni kazi ngumu, lakini tulijitahidi kwa kila namna. Mpango wetu wa kiufundi ulikuwa mzuri, tulitaka kuwazuia kwa sababu tunajua ubora wao. Penalti waliyopata ilibadili kabisa sura ya mchezo, lakini hata hivyo tuliwapambana hadi mwisho.”
Kwa upande wake, kocha wa Algeria, Vladimir Petković, alisifu mapambano ya pande zote mbili akisema “Ilikuwa mechi ngumu sana kati ya timu mbili zenye nguvu, kila mmoja akipigania kila mpira kwa dakika 90. Tulikuwa bora kidogo katika kutumia nafasi tuliyopata. Burkina Faso wanaweza kufanikiwa kama wataendelea kucheza kwa kiwango walichoonyesha leo. Hongera kwa timu yangu kwa kazi kubwa na kwa kufuzu.”
Kwa ushindi huu, Algeria wametuma ujumbe mzito kwa wapinzani wao kuwa wapo tayari kupigania taji, huku macho ya mashabiki yakisubiri kwa hamu kuona hatma ya Kundi E itakavyokuwa katika michezo ya mwisho ya mkesha wa Mwaka Mpya.

