Anthony Joshua Apata Ajali Nigeria

Bondia maarufu wa uzito wa juu kutoka Uingereza, Anthony Joshua, amejeruhiwa katika ajali mbaya ya gari iliyotokea nchini Nigeria, ajali iliyosababisha vifo vya watu wawili waliokuwa sehemu ya timu yake ya karibu. Tukio hilo la kusikitisha limetokea katika Jimbo la Ogun, karibu na jiji la Lagos, na limeutikisa ulimwengu wa ndondi pamoja na mashabiki wa AJ duniani kote.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Joshua, ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia, alikuwa abiria ndani ya gari aina ya Lexus SUV lililokuwa likisafiri katika barabara kuu (expressway) kutoka Lagos kuelekea Sagamu. Gari hilo liligongana na lori lililokuwa limesimama pembeni ya barabara, hali iliyosababisha ajali hiyo mbaya.
Watu wawili waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Sina Ghami na Latif “Latz” Ayodele, ambao walikuwa marafiki wa karibu sana wa Anthony Joshua na pia wajumbe muhimu wa timu yake. Taarifa ya vifo vyao imethibitishwa na kampuni ya Matchroom Boxing, ambayo ndiyo promota wa Joshua.

Matchroom Boxing ilisema katika taarifa yake kuwa Joshua alikimbizwa hospitalini mara baada ya ajali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu. Iliongeza kuwa bondia huyo yupo katika hali nzuri (stable) na ataendelea kubaki hospitalini chini ya uangalizi wa madaktari kwa muda ili kuhakikisha afya yake iko salama.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usimamizi na Utekelezaji wa Sheria za Usalama Barabarani nchini Nigeria (TRACE), Babatunde Akinbiyi, alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa gari la Lexus lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi kupita kiasi. Alieleza kuwa gari hilo lilipasuka tairi ghafla, jambo lililosababisha dereva kupoteza mwelekeo na hatimaye kugongana na lori lililokuwa limesimama barabarani.
Akinbiyi alisema Anthony Joshua na dereva wa gari waliokolewa kutoka kwenye mabaki ya gari hilo na kupelekwa hospitali moja mjini Sagamu kwa ajili ya matibabu. Kwa masikitiko makubwa, Sina Ghami na Latif Ayodele walitangazwa kufariki dunia papo hapo katika eneo la tukio.

Taarifa ya Matchroom Boxing ilieleza huzuni kubwa waliyonayo kufuatia msiba huo mzito. “Rambirambi zetu za dhati na sala zetu ziko pamoja na familia, marafiki na wote walioathirika na tukio hili. Tunaomba faragha yao iheshimiwe katika kipindi hiki kigumu sana,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mwenyekiti wa Matchroom Boxing na promota maarufu wa ndondi, Eddie Hearn, alitoa salamu za pole na kuwaomboleza waliopoteza maisha. “Pumzikeni kwa amani ya milele Sina na Latz. Mawazo na sala zangu za dhati ziko pamoja na kila mmoja katika wakati huu mgumu,” alisema Hearn.
Mtaalamu wa masuala ya ndondi, Steve Bunce, aliwataja Sina Ghami na Latif Ayodele kuwa ni watu wawili waliokuwa karibu mno na Anthony Joshua, na waliokuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya bondia huyo. Akizungumza na BBC Radio 5 Live, Bunce alisema wawili hao walikuwa sehemu kubwa ya mfumo mzima wa Joshua ndani na nje ya ulingo.
“Wamekuwa naye kwa muda mrefu sana, kama si tangu mwanzo basi tangu hatua za awali kabisa za safari yake ya ndondi. Latz alikuwa mkufunzi binafsi wa Joshua, wakati Sina alikuwa mtaalamu wa nguvu na mazoezi ya viungo. Walikuwa naye karibu kila wakati,” alisema Bunce.
Kwa upande mwingine, tukio hilo limezidisha majonzi baada ya kubainika kuwa saa chache tu kabla ya ajali, Anthony Joshua alikuwa ameweka video katika ukurasa wake wa Instagram ikimuonyesha yeye na Latif Ayodele wakicheza mchezo wa mezani (table tennis), wakionekana wenye furaha na afya njema. Sina Ghami pia alikuwa ameweka chapisho katika mitandao ya kijamii akiwa Lagos siku chache kabla ya ajali hiyo.
Habari za ajali hiyo zimepokelewa kwa mshtuko mkubwa na mashabiki wa michezo duniani, hususan wapenzi wa ndondi, ambao wamekuwa wakituma salamu za pole na dua kwa familia za marehemu pamoja na kumtakia Anthony Joshua uponaji wa haraka.
Tukio hili limeacha pengo kubwa katika maisha ya Joshua, si tu kama bondia, bali pia kama binadamu aliyepoteza watu aliokuwa nao karibu kila siku. Dunia ya michezo sasa inasubiri kwa matumaini kuona nyota huyo wa ndondi akipona haraka, huku ikiomboleza vifo vya watu wawili waliokuwa sehemu muhimu ya safari yake ya mafanikio.

