Yanga Sc Yamtambulisha Okelo

Klabu ya Yanga Sc imethibitisha rasmi kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Allan Okello (25), kwa mkataba wa miaka miwili na nusu utakaomalizika Juni 30, 2028, hatua inayotafsiriwa kama ushindi mkubwa katika dirisha la usajili huku ikionyesha dhamira ya klabu hiyo kuendelea kutawala soka la ndani na kufanya vizuri kimataifa.
Okello anajiunga na Yanga akitokea Vipers SC ya Uganda, ambako msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Uganda (UPL) 2024/2025 aliandika historia kwa kuibuka mfungaji bora wa ligi baada ya kufunga mabao 19, sambamba na kutoa pasi nne za mabao (assist), hivyo kuhusika moja kwa moja kwenye jumla ya mabao 23 kwa klabu yake. Ufanisi huo ulimweka katika rada za klabu kadhaa barani Afrika, lakini Yanga imefanikiwa kunasa saini yake.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za ndani ya soka, Yanga imelipa takribani Dola za Marekani 300,000 (zaidi ya Sh milioni 750) kama ada ya uhamisho kwa Vipers SC, huku Okello akipokea Dola 100,000 kama ada ya kusaini (sign-on fee). Aidha, nyota huyo anatajwa kuweka mfukoni Dola 15,000 kwa mwezi kama mshahara wake mpya, jambo linalomweka miongoni mwa wachezaji wanaolipwa vizuri zaidi katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mbali na mafanikio yake ya ngazi ya klabu, Okello ni nguzo muhimu ya timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes, akiwa ameichezea mara 36, akifunga mabao sita na kutoa assist 10. Takwimu hizo zinaonyesha mchango wake mkubwa katika safu ya ushambuliaji na ujenzi wa mashambulizi, hasa kutokana na uwezo wake wa kucheza kama kiungo mshambuliaji (namba 10) au winga anayeingia katikati.

Yanga, kupitia taarifa yake ya utambulisho, imemsifu Okello kama mchezaji mwenye nidhamu ya hali ya juu, sifa ambayo imejidhihirisha wazi katika taaluma yake. Rekodi zinaonyesha kuwa hajawahi kuonyeshwa kadi yoyote akiwa na jezi ya timu ya taifa ya Uganda, huku katika ngazi ya klabu hajawahi kupata kadi nyekundu na ameonyeshwa kadi tatu tu za njano tangu aanze kucheza soka la ushindani. Hii ni ishara ya ukomavu, nidhamu na uwezo wa kucheza kwa akili, vitu ambavyo Yanga imekuwa ikivipa kipaumbele katika usajili wake wa hivi karibuni.
Okello ni zao la kituo cha kulelea vipaji cha KCCA FC, moja ya klabu kubwa nchini Uganda inayojulikana kwa kuibua vipaji vingi vilivyotamba Afrika Mashariki na nje ya mipaka. Akiwa KCCA, alionesha dalili za ubora wake mapema kabla ya kuhamia Vipers SC, ambako alikua zaidi na kupevuka kisoka, jambo lililompa nafasi ya kuwa mfungaji bora wa ligi.
Kwa Yanga, ujio wa Okello unaongeza ubunifu, mabao na uzoefu wa kimataifa katika kikosi chake, hasa ikizingatiwa malengo ya klabu hiyo katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) pamoja na kutetea ubingwa wa ndani. Mashabiki wa Yanga wanatarajia Okello kuunda ushirikiano mzuri na nyota wengine wa kikosi hicho, wakiamini kuwa ataongeza chaguo la mbinu kwa benchi la ufundi.
Akizungumza mara baada ya kutambulishwa, Okello alinukuliwa akieleza furaha yake kujiunga na Yanga, akisema ni klabu kubwa yenye historia na mashabiki wengi, huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii na kutoa kila alicho nacho ili kuisaidia timu kufikia malengo yake. βNimefurahi sana kuwa sehemu ya familia ya Yanga. Najua matarajio ni makubwa, lakini niko tayari kwa changamoto,β alinukuliwa Okello.
Kwa upande wao, viongozi wa Yanga wamesisitiza kuwa usajili wa Okello ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha kikosi kwa wachezaji wenye ubora, nidhamu na njaa ya mafanikio. Wameeleza kuwa imani waliyonayo kwa mchezaji huyo imetokana na takwimu zake, tabia yake uwanjani na uzoefu wake katika mashindano ya kimataifa.

Kwa jumla, dili la Allan Okello linatajwa kuwa mojawapo ya usajili mkubwa katika soka la Tanzania kwa msimu huu, si tu kwa thamani ya fedha iliyotumika, bali pia kwa ubora wa mchezaji mwenyewe. Macho sasa yako uwanjani kusubiri kuona kama nyota huyo wa Uganda ataweza kuhamisha makali yake kutoka UPL kwenda Ligi Kuu Tanzania Bara na kuwa kipenzi kipya cha mashabiki wa Jangwani.
SIMBA YAMKOSA OKELLO, YANGA YAINGIA KATI NA KUNASA SAINI
Chanzo cha kuaminika cha ndani ya mchakato wa usajili kimedai kuwa Simba SC iliwasilisha ofa ya awali kwa klabu ya Vipers SC ya Uganda kwa ajili ya mchezaji huyo, hata hivyo ofa hiyo ilitajwa kuwa ndogo kulingana na thamani na mchango wa Okello ndani ya kikosi cha Vipers. Kufuatia hilo, Vipers waliomba Simba waongeze kiasi cha fedha na wakaweka muda wa wiki mbili kwa klabu hiyo ya Msimbazi kukamilisha na kuwasilisha ofa mpya iliyoboreshwa.
Taarifa zinaeleza kuwa, wakati huo huo, tayari kulikuwa na maongezi ya ana kwa ana kati ya Simba SC kupitia kwa Mwenyekiti wake na timu ya mchezaji, mazungumzo ambayo yalielezwa kuwa yalikuwa mazuri na yenye mwelekeo chanya. Chanzo kimesisitiza kuwa Allan Okello mwenyewe alionyesha nia ya kujiunga na Simba SC, akivutiwa na historia ya klabu hiyo na fursa ya kucheza mashindano ya kimataifa.
Hata hivyo, Simba ilishindwa kuwasilisha ofa ya pili ndani ya muda uliotolewa. Chanzo kimeeleza kuwa miongoni mwa sababu kubwa zilizoikwamisha Simba ni changamoto ndani ya kamati ya usajili, ambayo ilishindwa kufanya maamuzi ya haraka kuhusu ni mchezaji gani wa kimataifa kati ya 12 waliokuwapo angeachwa ili kupisha usajili wa Okello.
Baada ya Simba SC kushindwa kutuma ofa ya ongezeko la pesa kwa wakati, ndipo Rais wa Yanga, Eng. Hersi Said, alipoingia kati kwa kasi, akaendesha mazungumzo kwa ufanisi na hatimaye akaondoka na saini ya Allan Okello, akiipa Yanga ushindi mkubwa sokoni.
