Folz Afunguka Kilichomtoa Yanga Sc

Kocha wa zamani wa Young Africans SC, Romain Folz, amevunja ukimya na kufichua kwa kina sababu zilizopelekea kuachana kwake na klabu hiyo Oktoba 18, 2025, akidai kuwa kuondolewa kwake hakukutokana na matokeo mabaya uwanjani, bali changamoto na misukosuko ya ndani ya klabu aliyodai haingeweza tena kuivumilia.
Akizungumza na Jarida la KICKOff katika toleo lake la Januari, Folz amesema maisha ndani ya Yanga yalikuwa magumu kwake pamoja na benchi lake la ufundi, hali aliyosema ilivuruga moja kwa moja mazingira ya kazi na maandalizi ya timu, licha ya wao kutimiza majukumu yao kwa kiwango cha juu.
Kocha huyo raia wa Ufaransa, aliyefanikiwa kutwaa taji moja wakati wa kipindi chake Jangwani, alisisitiza kuwa kufukuzwa kwake kulikuja kwa kushangaza, hasa ikizingatiwa kuwa alitimuliwa baada ya kupoteza mchezo mmoja pekee tangu aanze kazi hiyo.
“Ninafanya kazi ili kushinda, na kukusanya mataji huwa ni jambo zuri kila wakati. Lakini kufukuzwa kwangu hakukuwa kwa sababu ya soka au matokeo. Kulikuwa na upuuzi mwingi nje ya uwanja ambao mimi na benchi langu la ufundi tulilazimika kuupitia kila siku,” alisema Folz.
MAANDALIZI YALIVURUGWA
Folz amesema moja ya changamoto kubwa zilizomsumbua ni kile alichokiita kuvurugwa kwa maandalizi ya timu, jambo alilodai lilikuwa linatokana na maamuzi ya ndani ya klabu ambayo hayakufuata misingi ya kitaalamu.
Kwa mujibu wa kocha huyo, alijaribu kupinga hali hiyo kwa nguvu zote kwa maslahi ya timu, lakini juhudi zake hazikupata uungwaji mkono wa kutosha.

“Maandalizi yetu yalivurugwa sana ndani ya klabu. Nilipinga hali hiyo waziwazi kwa sababu nilijua inaiumiza timu. Bila matatizo hayo, nisingepoteza hata mchezo mmoja, naweza kukuhakikishia hilo,” aliongeza.
Kauli hiyo imezua mjadala mpana miongoni mwa wadau wa soka nchini, hasa ikizingatiwa kuwa Yanga ni moja ya klabu kubwa zenye matarajio makubwa ya mafanikio ya haraka, hali inayoweka presha kubwa kwa makocha wanaofanya kazi ndani ya mfumo huo.
KIPIGO KIMOJA, MWISHO WA SAFARI
Folz ameeleza kushangazwa na uamuzi wa klabu kumuondoa madarakani mara baada ya kipigo chake cha kwanza na cha pekee, akisema hakikuwa kipigo cha aibu wala kilichoashiria kuporomoka kwa timu.
“Nilifukuzwa baada ya kipigo changu cha kwanza na cha pekee. Tulifungwa bao moja tu kwa jumla. Kipigo hicho hakikuhusiana na mimi wala benchi langu la ufundi,” alisema kwa msisitizo.
Kwa mujibu wa takwimu, katika kipindi chake klabuni hapo, Folz aliiongoza Yanga katika mechi kadhaa bila kupoteza, huku timu ikionyesha nidhamu ya kiufundi na uimara wa kimbinu, hali iliyowafanya baadhi ya wachambuzi wa soka kuhoji uamuzi wa kumuondoa mapema.
BENCHI LA UFUNDI LILITIMIZA WAJIBU
Kocha huyo ameweka wazi kuwa hana shaka na kazi iliyofanywa na yeye pamoja na benchi lake la ufundi, akisema waliitimiza dhamana yao ipasavyo kwa kuzingatia malengo waliyopewa.
“Mimi na benchi langu la ufundi tulitimiza wajibu wetu. Tulifanya kazi kwa weledi, nidhamu na kwa lengo la kuipa Yanga mafanikio ya muda mrefu,” alisema.
Kauli hiyo imewapa nguvu wale wanaoamini kuwa changamoto za baadhi ya klabu kubwa barani Afrika hazipo ndani ya uwanja pekee, bali pia katika mifumo ya uendeshaji na maamuzi ya kiutawala.
SOMO KWA SOKA LA TANZANIA
Kauli za Folz zimefungua mjadala mpana kuhusu umuhimu wa kuweka mazingira rafiki kwa makocha na benchi za ufundi ili kufanikisha malengo ya timu. Wadau wengi wanaamini kuwa ili klabu za Tanzania ziendelee kupiga hatua kimataifa, lazima ziwe tayari kulinda misingi ya kitaalamu na kumpa kocha muda na uhuru wa kufanya kazi yake.
Kwa upande wa Yanga, klabu haijatoa majibu rasmi kufuatia kauli za kocha huyo wa zamani, lakini tukio hilo linaendelea kubaki kuwa sehemu ya historia ya klabu hiyo yenye mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi.
Kwa Folz, ukurasa wa Yanga umefungwa, lakini maelezo yake yanaacha maswali mazito kuhusu nini hasa hufanyika nyuma ya pazia katika moja ya klabu kubwa zaidi Afrika Mashariki.
