Kumekucha Simba Sc

Timu ya maisha yetu. NguvuMoja

Klabu ya Simba SC imeanza rasmi mchakato wa kukifanyia marekebisho kikosi chake kuelekea muendelezo wa mashindano ya ndani na kimataifa, hususan Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League), kwa kuwapa kazi mawakala kuwatafutia timu za kuwatolea kwa mkopo baadhi ya wachezaji wake wa kigeni, huku ikikamilisha pia usajili wa mshambuliaji Baraka Mwangosi kutoka Mbeya City.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, uongozi wa Simba una mpango wa kuwatoa kwa mkopo wachezaji wanne wa kigeni, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa wachezaji wa nje na kutoa nafasi kwa usajili mpya unaotarajiwa kufanywa dirisha hili dogo.

Mazoezi mepesi. MapinduziCup2026 NguvuMoja

Miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye orodha ya kutolewa kwa mkopo ni beki Chamou Karabou, mshambuliaji Steven Mukwala pamoja na kiungo Joshua Mutale, ambao kwa sasa hawapo kwenye mipango ya moja kwa moja ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha mkuu Steven Barker.

Chanzo cha karibu na klabu hiyo kimesema kuwa uamuzi wa kuwatoa wachezaji hao umetokana na tathmini ya kiufundi iliyofanywa na benchi la ufundi, likilenga kuongeza ushindani na ufanisi katika kikosi kikuu.

“Ni maamuzi ya kiufundi. Simba inahitaji wachezaji watakaoweza kutoa mchango wa haraka na thabiti, hasa kwenye mashindano ya kimataifa,” kilisema chanzo hicho.

NEO MAEMA KUREJEA?

Katika mabadiliko hayo, imeelezwa kuwa kiungo mshambuliaji Neo Maema anaweza kurejea katika klabu aliyotoka awali, ikiwa sehemu ya mipango ya kupisha usajili mpya wa wachezaji wa kigeni. Hata hivyo, suala hilo bado liko katika hatua za awali za majadiliano.

Kocha Barker tayari ana wachezaji wawili wa kigeni anaowahitaji kuendelea nao, huku viongozi wa Simba wakipambana kuhakikisha wanakamilisha usajili wa wachezaji wawili wengine wa kigeni pamoja na mlinda mlango, ili kukamilisha kikosi chenye ushindani mkubwa.

NYOTA AFCON WARUDI MAZOEZINI

Wakati mchakato huo wa usajili ukiendelea, Simba SC haikupoteza muda kuanza maandalizi ya CAF Champions League. Wachezaji wake waliokuwa na kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki AFCON, wameanza kujiunga na wenzao katika mazoezi yaliyofanyika jana, Januari 11, 2026.

Nahodha Shomari Kapombe, pamoja na Seleman Mwalimu, Morice Abraham, Wilson Nangu na Yusuph Kagoma, wote walionekana uwanjani wakifanya mazoezi, ishara kuwa klabu hiyo haina mpango wa kutoa mapumziko marefu kwa nyota wake waliotoka AFCON.

Mchezaji pekee aliyekosekana katika mazoezi hayo ni Yakoub Suleiman, ambaye ni majeruhi na anaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa jopo la madaktari wa klabu.

Hatua ya kuwarejesha wachezaji hao mapema imeonyesha wazi msimamo wa Simba SC kwamba haina muda wa kupumzika, ikiwa na dhamira ya kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

MWANGOSI AINGIA RASMI

Katika habari nyingine njema kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi, klabu hiyo imethibitisha rasmi kumsajili mshambuliaji Baraka Mwangosi akitokea klabu ya Mbeya City, baada ya kumridhisha kocha na benchi la ufundi kupitia majaribio aliyofanya katika mashindano ya Mapinduzi Cup.

Siku nyingine kwenye uwanja wa mazoezi. NguvuMoja

Mwangosi, ambaye alikuwa akifanya majaribio kwa muda, alionyesha kiwango cha juu, utulivu mbele ya lango na uwezo wa kushirikiana na wachezaji wenzake, hali iliyowashawishi viongozi wa Simba kumchukua moja kwa moja.

Baada ya kukamilika kwa taratibu zote za usajili, Mwangosi sasa ni mchezaji halali wa Simba SC, hatua inayoongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Kocha Barker anaamini kuwa ujio wa Mwangosi utaongeza ushindani wa ndani, jambo linalotarajiwa kuongeza ufanisi wa timu katika mechi muhimu zijazo.

“Tunataka ushindani katika kila nafasi. Mwangosi ameonyesha anaweza kucheza katika mfumo wetu,” alisema mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi.

SIMBA YAPIGA KAZI KIMKAKATI

Kwa ujumla, hatua hizi zinaonyesha kuwa Simba SC ipo katika awamu ya mabadiliko ya kimkakati, ikilenga kuunda kikosi chenye uwiano sahihi wa wachezaji wa ndani na wa kigeni, pamoja na kuongeza ubora katika nafasi muhimu.

Mashabiki wa Simba sasa wanasubiri kwa hamu kuona wachezaji wapya watakaoletwa, pamoja na namna Mwangosi atakavyojumuishwa kwenye mfumo wa timu. Wakati huo huo, uamuzi wa kutowapa mapumziko nyota waliotoka AFCON unaashiria wazi kuwa malengo ya klabu hiyo msimu huu ni makubwa, na hakuna nafasi ya kulegeza kamba.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks