Yanga Sc Yaokota Alama Muhimu Algeria

Klabu ya Yanga SC imeendelea kuonyesha uimara na utulivu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baada ya kupata sare ya bila kufungana dhidi ya JS Kabylie ya Algeria, mchezo uliochezwa katika dimba la 1er Novembre 1954 jijini Tizi Ouzou. Sare hiyo imeifanya Yanga SC kufikisha alama nne katika michezo miwili ya awali, na kuendelea kuimarisha nafasi yao katika kundi B ambalo linaonekana kuwa na ushindani mkali msimu huu.
Katika mchezo huo uliosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa mpira wa miguu barani Afrika, kocha mkuu wa Yanga SC, Pedro Gonçalves, aliamua kuingia na kikosi kilekile kilichopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat wiki iliyopita. Mbinu hiyo ilionekana wazi kuwa ilikuwa ni ya kuendelea kujenga muunganiko kwenye maeneo yote ya uwanja, huku safu ya ushambuliaji ikiongozwa na Prince Dube na Mudathir Yahya. Wawili hao walikuwa wakipewa msaada wa karibu na washambulizi wa pembeni Pacome Zouzoua na Celestine Aucho (Ecua), pamoja na viungo mahiri Duke Abuya na Max Nzengeli.
Kama ilivyokuwa mchezo uliopita, Djigui Diarra alisimama langoni, huku safu ya ulinzi ikijengwa na mabeki Dickson Job, Ibrahim Hamad, Israel Mwenda na Mohammed Hussein “Tshabalala”. Ulinzi huo ulionekana kuzoea presha ya wenyeji mapema, licha ya JS Kabylie kuanza mchezo kwa kasi na ari ya kutaka kupata bao la mapema mbele ya mashabiki wao.
Yanga SC ilionyesha nidhamu ya hali ya juu katika eneo la kati, na mara kadhaa walikuwa wakifanya pressing ya juu ambayo iliizuia JS Kabylie kupanga mashambulizi yao kwa utaratibu. Utawala huo wa eneo la kiungo uliwapa nafasi wageni kuingia mara kwa mara katika eneo la hatari la wapinzani, ambapo Celestine Ecua alipata nafasi mbili muhimu, lakini hakuweza kuzigeuza kuwa mabao. Mudathir Yahya pia alipata nafasi ya kuandika bao, lakini shuti lake lilidakwa na kipa wa JS Kabylie.
Kadri mchezo ulivyoendelea, JS Kabylie waliongeza kasi na mashambulizi yao yalionekana kuongezeka hasa katika dakika za mwisho za kipindi cha kwanza, lakini ukuta wa Yanga SC ulisimama imara, huku Djigui Diarra akiendelea kuthibitisha ubora wake kwa kuokoa michomo kadhaa iliyokuwa ikivurumishwa kwa kasi.
Kipindi cha pili kilianza kwa kocha Pedro Gonçalves kufanya mabadiliko ya kimkakati, akimtoa Mudathir Yahya na kumwingiza Mohammed Doumbia. Lengo lilikuwa kuongeza utulivu na umakini sehemu ya kati, kwa kuwa wenyeji waliokaa nyuma kipindi cha kwanza walionekana kurudi uwanjani wakiwa na nguvu mpya za kushambulia. Doumbia aliingia vizuri katika mchezo na kusaidia kupunguza kasi ya mashambulizi ya JS Kabylie, lakini bado wenyeji waliendelea kutafuta bao kwa kusukuma wachezaji wengi mbele.
Hata hivyo, Yanga SC hawakubweteka. Walijibu kwa kufanya mashambulizi ya kushitukiza (counter attacks) yakiongozwa na Dube na Zouzoua, japokuwa mara kadhaa walikosa utulivu katika hatua ya mwisho. Mabadiliko zaidi yalifanyika dakika za mwisho ambapo Pedro aliwaingiza Chadrack Boka, Aziz Andabwile na Edmund John kuongeza nguvu, hasa katika eneo la kiungo ambalo lilikuwa linahitaji kasi zaidi kutokana na uchovu ulioanza kuonekana.
Kadri dakika zilivyoyoyoma, Yanga SC walionyesha ukomavu mkubwa wa kimchezo kwa kucheza kwa nidhamu, kusimama vizuri nyuma na kushambulia pale palipohitajika. Mwisho wa mchezo ukapisha sare ya 0-0, matokeo ambayo kwa kiasi kikubwa yanachukuliwa kama ushindi kwa mchezo wa ugenini katika moja ya viwanja vigumu zaidi Afrika Kaskazini.
Kwa matokeo hayo, Yanga SC inafikisha alama nne na kwa muda iliongoza kundi B kabla ya Al Ahly kutoka sare ya 1-1 dhidi ya AS FAR Rabat. Hadi sasa, Al Ahly wana alama nne sawa na Yanga, wakati FAR Rabat na JS Kabylie wanabaki na alama moja moja.
Sare hiyo ni ishara kuwa Yanga SC imekuja na sura mpya msimu huu, ikionyesha kupambana, nidhamu na kujiamini uwanjani – sifa ambazo zinaweza kuwafikisha mbali zaidi katika hatua za makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika.



